• Breaking News

  Oct 17, 2016

  Lowasa Jifunze kwa Dr Slaa

  Dk Willibrod Slaa aliposhawishiwa kugombea urais mwaka 2010 alipokuwa Chadema, alipambwa na kila aina ya sifa. Hata baada ya kushindwa, walimwita rais wa mioyo ya Watanzania.

  Chadema walimwonesha Dk Slaa mapenzi makubwa na yeye aliyaona. Mwaka 2015 walitofautiana, Chadema haohao walimwonesha chuki kubwa na yeye aliiona.

  Walipompenda walimwita Rais wa Mioyo ya Watanzania, walipomchukia walimwita msaliti, mwanaume anayetawaliwa na mkewe, vilevile aliyehongwa mabilioni na CCM.

  Ngoja nikwambie; Mapenzi ya wanasiasa wa Chadema kwa Slaa yalikuwa ya fursa. Hayakuwa mapenzi ya moyoni. Ndiyo maana kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, walimfanyia mabadiliko (sub) ya juu kwa juu, baada ya kuona usajili wa Edward Lowassa kutoka CCM, ulikuwa fursa kubwa zaidi.

  Lowassa alibeba matumaini makubwa ya Chadema pamoja na vyama vya Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD kupitia muungano wao wa Ukawa, kwa hiyo yeyote yule ambaye alikuwa anaenda kinyume naye kwenye vyama hivyo, alijikuta akiumizwa vibaya.

  Kama Prof Ibrahim Lipumba ndivyo ilivyo kwa Dk Slaa, walipendwa kwa fursa na wametoswa kwa sababu ya fursa kwa Lowassa. Siku Lowassa naye ataonekana siyo fursa, mapenzi yatakoma au kuhamia kwa mwingine.

  Lowassa alikuwa na watu wengi CCM lakini alihama na wachache, ni kwa sababu aliokuwa nao CCM waliamini ni rais ajaye, kwa hiyo wakampenda kwa kumuona ni fursa yao.

  Waliobaki CCM na kumuacha Lowassa akihamia Chadema na Ukawa, walifanya hivyo kwa kuona kuwa fursa ni kidogo, kwamba alikuwa na nafasi finyu ya kuishinda CCM na kushinda urais. Fursa za kisiasa huchochea mapenzi kwa wanasiasa, huyafifisha yaliyokuwepo, vilevile kuibua chuki palipokuwa na upendo.

  NAZIDI KUKUMBUSHA

  Wanasiasa hupendana kwa maslahi na huchukiana kwa maslahi. Siku zote uwe makini unapopendwa na mwanasiasa. Ukichukiwa na mwanasiasa ujue unaingilia maslahi yake.

  Chukua hii; Katika siasa fursa huleta upendo, vilevile fursa huzalisha chuki.

  Ndimi Luqman Maloto

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku