• Breaking News

  Oct 9, 2016

  Mvutano wa Siasa Zanzibar...CUF Yatoa Masharti Mawili Kwa Serikali

  Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii katika mahojiano maalumu mjini Zanzibar juzi, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema masharti hayo mawili yanayopaswa kuzingatiwa ni kuhakikisha kuwa panaundwa Serikali ya Mseto na jambo la pili, ni sharti kwa serikali hiyo kuandaa uchaguzi mwingine visiwani humo utakaotoa fursa ya wananchi kujichagulia kwa uhuru viongozi wanaowataka.

  Aliyekuwa mgombea wa CUF katika uchaguzi mkuu uliopita, Maalim Seif Shariff Hamad, aliwaambia waandishi wa habari siku chache baada ya uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015 kuwa anaelekea kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutenda haki. Hata hivyo, ilipofika Oktoba 28, 2015, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufutwa kwa uchaguzi huo kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa kasoro nyingi.

  Uamuzi huo wa Jecha ulipingwa na CUF na pia waangalizi mbalimbali wa ndani na wa kimataifa. Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016, CUF iligoma kushiriki na kuitaka ZEC iendelee na majumuisho ya kura zilizotokana na uchaguzi wa Oktoba 25. Matokeo ya uchaguzi wa marudio yakaonyesha kuwa mgombea wa CCM, Rais Shein, ameshinda kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura halali zilizopigwa.

  Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa CCM na CUF kurudi mezani na kufanya mazungumzo kwa nia ya kuona kuwa Zanzibar haiwi na mvutano wa kisiasa unaoelekea kuwagawa watu kiitikadi, Jussa alisema hilo ni jambo zuri na wao siku zote wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa siasa za mazungumzo na siyo za kuegemea matumizi ya “nguvu na mabavu”.

  “CUF siku zote imekuwa mstari wa mbele. Haijawahi kukataa mazungumzo hata siku moja kwa sababu tunaamini kuwa siasa inafanywa kwa mazungumzo, siyo kwa kutumia mabavu na vitisho, hayo yamepitwa na wakati katika dunia ya leo,” alisema Jussa na kuongeza:

  “Na niseme kwamba pamoja na kuamini kuwa tumeshinda kihalali katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, bado CUF imenyoosha mkono na kutoa mapendekezo kupitia kiongozi wetu Maalim Seif Sharif Hamad, hasa akiwa katika ziara nchi za nje, kutaka pafanyike mazungumzo yatakayowezesha kuundwa kwa Serikali ya Mpito na baadaye kukubaliana juu ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.”

  Akieleza zaidi, Jussa alisema wapo wananchi ambao hadi sasa wangali na kinyongo kutokana na kukasirishwa na hila zilizofanyika katika uchaguzi mkuu uliopita.

  “Siyo kama watu hawazikani, wapo wananchi wamekasirishwa mno na kitendo kilichofanyika kwa sababu hawakutarajia Zanzibar kurejeshwa ilipotoka…hawaipi ushirikiano Serikali. Bila shaka pana haja ya mazungumzo lakini ili mazungumzo hayo yafanyike panahitajika kwanza kutambua tatizo kwa pande zote mbili zinazohasimiana. Pili kuwe na utashi wa kuona kuwa mazungumzo hayo yanaleta tija.

   “Na ndio maana sisi CUF tunasema kwamba mazungumzo kati ya CCM na CUF tumeshafanya mengi lakini hayaonekani kwamba yanachukuliwa kwa umakini, kuna haja ya kuwa na mpatanishi ambaye atasimamia mazungumzo hayo na awe mtu anayeheshimika na mwenye uadilifu, atoke nje ya Tanzania au nje ya Afrika.”

  Aidha, Jussa alisema Zanzibar ni ya wananchi wote wa Zanzibar bila kujali itikadi za vyama na hivyo, kuendelea kuvutana hakuwanufaishi wananchi.

  “Kwa upande wa Bara wanapaswa kutambua kuwa hali inayoendelea sasa haina maslahi hata katika Muungano…muungano hauwezi kujengwa kwa kuidhoofisha Zanzibar. Tunapaswa tushirikiane ili Zanzibar iwe imara, yenye umoja na mshikamano,” alisema Jussa

   – Nipashe

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku