• Breaking News

  Oct 17, 2016

  Mwanamke Mwenye Wivu ni Mchunguzi Hatari

  Ni usemi maarufu uliotungiwa kitabu na kuchezwa katika filamu, kuwa mwanamke mwenye wivu ni mpelelezi mzuri na mweledi kuliko polisi au afisa mpelelezi, hasa linapokuja suala la kufahamu mumewe, mpenzi wake anachepuka na nani?

  Mwanamke mwenye wivu anaweza kupata taarifa zote za mpinzani wake ndani ya dakika tano tu.

  Kengele ya hatari itakapogonga kichwani kuhusu mwizi wake, atamsaka katika mtandao wa Facebook, Instagram, Twitter na kupiga simu kwa watu anaowaamini...ndani ya dakika tano taarifa zote anazo mkononi.

  Utakapomsikia mwanamke anakwambia nataka tuzungumze kuhusu fulani, jua taarifa zote anazo mkononi.

  Utafiti

  Kuna tafiti nyingi na ushuhuda unaodhihirisha hilo, huku katika jamii zetu kila kukicha tukishuhudia ugomvi, kelele, malumbano baada ya wanawake kufanikiwa kubaini walichokuwa wakikitafuta muda mrefu.

  Utafiti uliofanywa na kampuni inayojihusisha na msaada ya sheria ya nchini Australia Slater & Gordon, unaonyesha namna ambavyo wanawake wanaweza kuwa wachunguzi wazuri kuliko polisi au shirika la upelelezi linapokuja suala la mapenzi.

  Katika kisa kimojawapo kinacholibainisha hilo ni mwanamke anapoamua kupoteza muda mrefu kutafuta ukweli ili umuweke huru.

  Mwanasheria wa familia wa kampuni iliyofanya utafiti huo Kaleel Anwar anasema wanawake sita kati ya 10 hutumia mitandao ya kijamii kufuatilia nyendo za waume zao. “Huunganisha matukio kwa kutizama ujumbe wanaotumiana kupitia mitandao ya kijamii. Wapo makini na upelelezi wao.”

  Mchunguzi

  Magdalena Luisou anasema aliwahi kubaini mumewe ana mpenzi wa nje kwa kuunganisha mawasiliano yao katika mtandao wa Facebook.

  Anasema kila mumewe alipokuwa akichangia mada kwenye mtandao huo, mwanamke huyo alichangia.

  “Niliingia kwenye ukurasa wake na kukuta miongoni mwa rafiki zake na wa karibu mume wangu yumo, kazi anayofanya ni tofauti na mume wangu, alikosoma pia ni tofauti, sikuona sababu iliyowafanya wawe karibu kiasi hicho nikatia shaka na kuazimia kufuatilia, ” anasema Luisou.

  Hivyo akatafuta namba ya msaidizi wa mumewe wa ofisini na kumpigia mara kwa mara kwa ajili ya salamu kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kuanza kumpeleleza, kama miongoni mwa wageni wanaofika ofisini kumtembelea yupo wa wajihi kama wa huyo dada anayemuhisi.

  Hakupata jibu la moja kwa moja zaidi ya kuendelea kuhisi hisi, “Nikamwambia mume wangu akitoka aniambie na ninapomuona yupo mtandaoni najua anachati na kumuuliza msaidizi wake kama yupo ofisini, siku ya kwanza alinijibu yupo na siku ya pili akasema ametoka muda siyo mrefu na baada ya muda akatoweka hewani, ”anasema.

  Anasema kwa muunganiko huo na salamu alizoona wamepeana kwenye facebook asubuhi akafahamu watakuwa wote wamepumzika mahali.

  Anasema alipompigia simu hakupokea, kwa kuwa alikuwa namba za yule dada nae alipompigia hakupokea.

  Anafafanua kuwa aliamua kuweka kambi ya siri kwa kujificha karibu na ofisini kwa mumewe kwa kukaa sehemu iliyomuwezesha kuona kila anayeingia na kutoka, japo ilikuwa taabu kidogo kutokana na kuwa na watu wengi.

  “Siku moja kwa mshangao mkubwa taksi ilisimama na aliyeshuka alikuwa ni yule dada anayemuhisi akiwa na begi na kukaa nje kwa muda kabla ya mumewe kutoka na wote kuingia kwenye gari ya mumewe na kuondoka, ”anasema.

  Hawawezi kuwaacha

  Utafiti huo wa Slater & Gordon umeonyesha zaidi ya asilimia moja kwa kila wanawake sita wanasema hawawezi kuwaacha waume zao hata wakigundua wanawasaliti kimapenzi.

  Pia umeonyesha kuna tofauti ya kuaminiana kati ya wanawake na wanaume ambapo asilimia 36 ya wanawake na asilimia 24 ya wanaume wanadhani wapenzi wao sio waaminifu, huku asilimia moja kati ya sita huangalia historia za wapenzi wao ikiwamo katika simu, kompyuta.

  Umeonyesha pia asilimia 10 ya wanawake hupiga simu ofisini kwa wame zao kuwauliza wasaidizi wao kama kweli wapo kazini.

  Asilimia 30 wanakiri kuwa licha ya kuwafuatilia wame zao kwa muda mrefu hawajabahatika kuwafuma, huku asilimia 70 wakisema kuwa hawajawahi kukosea kuwafuma ikiwa ni pamoja na wanapokuwa wametoka kwa ajili ya chakula, semina, hotelini kwa ajili ya mapumziko.

  Halima Yahaya anasema siyo kazi ngumu kugundua tabia mpya za mumewe kutokana na kumfuatilia.

  Anasema akirudi kazini kwa kumtizama na kusikia sauti yake hugundua kama ana tatizo na akifanya nae mahojiano machache hugundua kama ni la kiofisi au binafsi, ingawa huwa ngumu kugundua kama ni binafsi ni lipi hasa.

  “Kwa kuwa kila siku nahisi naibiwa mara nyingi huwa nafikiria fikiria ameudhiwa na mwanamke ndiyo maana amerudi muda huo, ”anasema.

  Anafafanua kutokana na tabia hiyo hata anapokuwa na uhusiano wa nje huwa rahisi kubaini hivyo huanza kufuatilia, ikiwamo alimbaini mumewe kwa njia hiyo.

  “Tulikuwa tunakula wote chakula cha jioni, ghafla akaanza kukataa na kusema atakula baadae”

  “Hilo lilinistua na kuanza kufuatilia kwa nini amebadili tabia ghafla” anasema.

  Anasema aliendelea kufuatilia na alipokuwa akiingia ndani kulala hafungi mlango vizuri anasikiliza nini kinaendelea sebuleni kwa sababu hawakuwa wengi alikuwa mtoto wao mmoja, msichana wa kazi na binamu yake aliyekuja kuwatembelea siku siyo nyingi.

  Anafafanua hali ya nyumba hiyo kuwa vyumba vyote vina milango kasoro cha wageni ambacho ndiyo alikuwa analala binamu yake.

  “Siku kama mbili hivi za kufuatilia nyendo zake nilibaini akinyata minyato yake huishi korido nikawa najiuliza inaishia wapi, nikaanza kufuatilia na kubaini inakosihia.

  “Nilisubiri ajisahau sebuleni, nikaingia kwenye chumba anacholala binamu yangu na kumnyamazisha kwa ishara ya kuweka kidole mdomoni na baada ya dakika 45 uchunguzi wangu ulitimia kwa sababu mume wangu waliingia na kujilaza pembeni ya binamu yangu bila kujua kama nipo, nikawasha taa na kumuumbua, ”anasema Yahaya.

  Yahaya anasema kwa ushahidi huo hakuwa na jinsi ya kukataa, lakini angemuuliza asingekubali.

  Mwanasaikolojia wa kampuni iliyofanya utafiti Bilgram Johnson anasema wanawake kwa kawaida wana uwezo zaidi wa kubaini mabadiliko ya wenza wao ukilinganisha na wanaume.

  Anasema utafiti huo ulibaini mwanamke ni ngumu kushtukiwa kama ameanza uhusiano sehemu na anapoulizwa swali lolote hujiuliza kwa nini kaulizwa hivyo kabla ya kujibu , ukilinganisha na wanaume ambao hujibu haraka na kuwarahisishia wanawake upelelezi wao.

  Utafiti huo uliohusisha madaktari wa afya, wataalamu wa saikolojia, wanasheria , ulibaini kuwa asilimia tano wanafahamu kumpeleleza mtu kwa siri ni kuingilia haki yake ya msingi, asilimia 17 walisema kufanya hivyo kunawapa amani ya nafsi na akili kuliko kuendelea kuhisi.

   By Kalunde Jamal

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku