• Breaking News

  Oct 8, 2016

  Ndanda yatishia kujiondoa Ligi Kuu


  Mtwara/Dar. Timu ya soka ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara, imetishia kujitoa katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inayoendelea kutokana na kukabiliwa na ukata.

  Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Idrisa Bandali alisema kuwa hali ya uchumi katika klabu hiyo ni ngumu hivyo watu wasishangae kuiona timu ikishindwa kuendelea na ligi.

  “Tuko katika wakati mgumu, hatuna fedha za kulipa wachezaji mishahara na hata shughuli za klabu na timu za kila siku.

  “Mfano mdogo tu, hivi karibuni tulilazimika kulala Dumila, Morogoro tukitokea Mwanza baada ya kuchelewa kuondoka kutokana na kukosa fedha ya kulipia hoteli.

  “Kuna wakati nimekuwa nikiomba wanahabari watusaidie kuifanya Ndanda kuwa ajenda katika vyombo vyao ili tupate msaada lakini hali bado ni mbaya.

  “Ninataka kuwaambia msishangae kuona Ndanda ikishindwa kuendelea na ligi licha ya kuwa bado tuna mechi za ugenini na tunafahamu tutakapokosa, adhabu mojawapo ni kushushwa daraja,” alisema Bandali.

  Kanuni za Ligi Kuu
  Kwa mujibu wa Kanuni ya 27 ya Ligi Kuu kifungu cha nne, klabu yoyote itakayojitoa kwenye Ligi Kuu baada ya Ligi kuanza au kushindwa kucheza mchezo mmoja wa ratiba ya Ligi Kuu katika msimu itakabiliwa na adhabu zifuatazo:

  (a) Itashushwa daraja na kufungiwa kucheza Ligi kwa misimu miwili, Bodi ya Ligi Kuu pia inaweza kuichukulia hatua zaidi klabu hiyo/viongozi au wachezaji iwapo itathibitika kuwa imejitoa kwa madhumuni ya kuhujumu msimamo wa Ligi au hujuma nyingine yoyote.

  (b) Iwapo itajitoa au kushindwa kumaliza Ligi kwa sababu yoyote ile, timu zaidi ya idadi ya timu za kushuka daraja kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, zote zitashuka daraja (kanuni 25:4a) na timu zaidi zitapanda kutoka daraja la kwanza (FDL) ili kujaza nafasi na idadi ya timu za Ligi Kuu kuendelea kuwa ilivyokusudiwa.

  Kipengele (c) kinasema matokeo ya michezo yote iliyowahi kuchezwa itafutwa lakini kitakuwepo kwenye orodha ya msimamo wa ligi.

  Kwa mujibu wa kanuni hizo kipengele (e), timu itapoteza haki zake zote stahili kwa timu za Ligi Kuu na itawajibika kurejesha stahili yoyote iliyokwishachukua kabla ya kujitoa endapo itaamriwa kufanya hivyo kutokana na mazingira ya kujitoa kwake.

  Licha ya kutoa tishio hilo huku ikicheza na African Lyon leo, Ndanda FC ilikwishacheza na Simba na kufungwa mabao 3-1, ilifungwa na Mbao FC mabao 2- 0 kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar.

  Mechi ambazo Ndanda yenye pointi 11, ilishinda ni dhidi ya Majimaji na Azam 2-1 na ile ya Toto Africans bao 1-0. Ndanda ilitoka suluhu mechi za Yanga na Kagera Sugar.

  “Kwa sasa hatuna mdhamini yoyote zaidi ya Azam anayedhamini ligi na kwamba tunaendeshwa kwa michango ya viongozi na wahisani mbalimbali ambao hujitolea kwa kiasi ambacho bado hakijitoshelezi.

  “’Kuendesha timu ni kazi ngumu, hali yetu ni mbaya ndio maana wakati mwigine tunashindwa kulipa mishahara kwani pia kuna wachezaji ambao bado hawajamaliziwa pesa za usajili zinazofikia Sh30mil kwa msimu huu wa 2016/2017,” alisema Bandali

  Ligi Kuu yaendelea
  Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ndanda FC, ligi hiyo inaendelea leo kwa Mtibwa Sugar kuwa ugenini dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi wakati Majimaji itaikaribisha Mbao kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

  Majimaji inayonolewa na Kally Ongalla, inashika mkia kwenye ligi na itakuwa na kazi ngumu leo kupambana na Mbao ambayo imeizinduka katika siku za karibuni.

  Ongalla alisema ana wakati mgumu kurejesha morali ya wachezaji wake ili warudi katika kiwango bora lakini anaamini mchezo wa leo watapata matokeo mazuri.

  Kocha wa Ndanda, Said Mohamed alitamba kuiadhibu Lyon kama alivyoifanyia Toto African wiki iliyopita.

  Naye kocha wa maafande wa JKT Ruvu, Malale Hamsini alisema anaijua shughuli ya Mtibwa Sugar hivi sasa na amekiri kuwa kazi itakuwepo leo huku Kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga akisema wamejindaa vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku