• Breaking News

  Oct 6, 2016

  UCHAMBUZI: Hongera Rais Magufuli Kwa Kukwepa Mtego huu

  Katika mambo ambayo najiuliza lakini sipati majibu yake, ni hatua ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kupendekeza ndege zetu mbili mpya ziitwe ‘Hapa Kazi Tu’.

  Kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, ilitumiwa na Rais John Magufuli katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, wakati huo Magufuli akipeperusha bendera ya CCM nafasi ya urais.

  Katika uzinduzi wa ndege hizo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jullius Nyerere (JNIA), Profesa Mbarawa alimuomba Rais Magufuli, aridhie ndege hizo zipewa jina la ‘Hapa Kazi Tu’.

  Profesa huyo ambaye binafsi naweza kusema alikuwa anajipendekeza kwa Rais, alienda mbali na kudai uamuzi wa kuzipa ndege hizo jina hilo ni mapendekezo ya pamoja na wenzake wizarani.

  Nilipomsikiliza Waziri huyo akitoa pendekezo hili la kuipa jina la ‘kisiasa’, ndege itakayotumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kujiendesha kibiashara, nilishtuka. Sikuamini nilichosikia.

  Kabla sijaeleza kwa nini sikubaliani na pendekezo hilo la Profesa Mbarawa, lazima nichukue fursa hii kumpongeza Rais Magufuli kwamba katika hotuba yake yote ya dakika 50 hakugusia pendekezo hilo.

  Rais alisema: “Hii ndege haikuandikwa CCM kwa hiyo meya hapa ataipanda, Mbowe (Freeman) ataipanda, CCM wataipanda, Lipumba (Ibrahim) ataipanda na asiye na chama ataipanda”.

  “Ni ndege za Watanzania na ni lazima tujifunze sisi Watanzania kujivunia utanzania wetu.” Alisisitiza Rais Magufuli, kauli ambayo ilionekana kujibu ombi la Profesa Mbarawa japo siyo moja kwa moja.

  Ndege hizi ni za Watanzania na zimenunuliwa kwa fedha za Watanzania wote pasipo kuingiza itikadi za kisiasa. Namshukuru na kumpongeza Rais wangu kwa kutoingia katika mtego huu wa Profesa Mbarawa.

  Nilijiuliza maswali mengi, hivi kama Rais mstaafu Jakaya Kikwete, angekuwa amefanikiwa kununua ndege katika kipindi chake nazo zingepewa jina la ‘Ari mpya, Kasi mpya na Nguvu mpya’?

  Hakuna tafsiri nyingine yoyote inayoweza kueleweka kwa nini Profesa Mbarawa aliamua kupendekeza jina hilo wakati akijua ndege hizi zinajiendesha kibiashara.

  Bahati nzuri katika kipindi kifupi nilichomfahamu Rais Magufuli anatanguliza utaifa na uzalendo kwanza na mambo ya vyama ni baadaye na hili amelithibitisha mara zote kwenye hotuba zake.

  Kwanini napinga jina la ‘Hapa Kazi Tu’? Ni dhana rahisi kwamba katika biashara ya usafiri wa anga ni lazima tuje na mkakati wa kuitangaza nchi na vivutio vyake, siyo itikadi za vyama.

  Tukitoa mfano, mdogo wa bidhaa. Huwezi amini kila mtalii aliyekuja kupanda Mlima Kilimanjaro au kutembelea mbuga za wanyama na kupewa orodha ya bidhaa atachagua zilizo na majina ya Kilimanjaro, Mikumi  au Serengeti.

  Ni kwa sababu ni vivutio maarufu duniani ambavyo vinatangazwa kimataifa, hivyo mtalii anapotumia bidhaa hizo anabaki na kumbukumbu ya hifadhi na vivutio alivyoviona Tanzania.

  Mara zote tunalalamika kuwa majirani zetu Kenya wanatangaza kimataifa kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya na hii imewafanya watalii wengi kushukia nchini humo badala ya Tanzania ulipo.

  Sasa leo badala ya kutumia fursa za uwapo wa ndege za ATCL ambazo baadaye zitafanya safari za kimataifa, kutangaza vivutio vyetu tunataka kutangaza ‘Hapa Kazi Tu’ ili tufanikiwe nini?.

  Binafsi naamini Menejimenti ya ATCL italifanyia kazi suala hilo na kuja na jina ambalo litasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

  By Daniel Mjema
  0769600900

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku