• Breaking News

  Oct 6, 2016

  UCHAMBUZI: Ukuta Umeipotezea Chadema Alama Nyingi

  Uamuzi ni kifo au uhai, unaweza kuleta faida au hasara, vilevile kujenga au kubomoa. Kila aina ya matokeo ni zao la uamuzi. Inategemea nini ambacho kiliamuliwa kisha kuleta matokeo husika.

  Ustawi wa chama cha siasa ni matokeo ya ujenzi wa taasisi, vilevile uamuzi ambao viongozi wake hufanya. Vyama vingi vya siasa havipo hai leo hii kwa sababu ya uamuzi.

  Uamuzi ili ulete matokeo chanya ni lazima uwe sahihi. Na uamuzi hauitwi sahihi mpaka uamuliwe katika wakati sahihi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya Uganda katika wakati sahihi ndiyo maana uamuzi ule umebaki kuwa sahihi.

  Chama cha siasa kwa ukuaji wake lazima kijue mazingira na wakati ili kifanye uamuzi sahihi. Siyo kwamba vyama vya siasa vilivyokufa havikuwa na watu wazuri, hapana, ila vilikosea katika uamuzi.

  Katika siasa ili chama kiitwe hai lazima kiwe na ufuasi. Wafuasi ndiyo huitwa wanachama na wakereketwa. Kumpata mkereketwa ni sharti hasa umkune kwa sera na matarajio. Ukimwonesha mwananchi matarajio yake, kweli atakipigania chama.

  Chama cha siasa kinapotaka kipotee haraka hata kama kinakubalika kiasi gani, basi kifanye uamuzi ambao hauendani na wakati. Kifo cha chama cha siasa ni kukimbilia kufanya uamuzi kabla hakijaufanyia tathmini kwa matokeo ya pande mbili, hasi na chanya.

  Mwongozo wa vyama vya siasa katika kufanya uamuzi wa matukio au ajenda, vinatakiwa kutumia mbinu ya kujichelewesha ili kujiridhisha kuhusu kesho. Ni dhambi kubwa kwa chama cha siasa kufanya uamuzi pasipo kufanya tathmini ya matokeo ya uamuzi wake.

  Angalizo kwa chama cha siasa ni kama benki; kibiashara inafahamika kuwa benki ikikosea katika uamuzi, inaweza kukera wateja ambao kesho wataamkia kwa watoa huduma na kuhamisha fedha zao. Vivyo hivyo kwa chama cha siasa, kikikosea na kuvunja moyo wanachama, kesho yake utakuta wanachama wanarudisha kadi.

  Kama ambavyo uamuzi wa benki huchukuliwa kwa kuzitangulia hisia za mteja, inatakiwa pia kwa chama, kumtazama mwanachama kabla ya kufanya uamuzi, maana yeye ndiye mwenye chama.

  Chadema na Ukuta

  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Julai mwaka huu kilitangaza kuunda Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

  Msimamo wao ukawa kwamba Septemba Mosi ingekuwa mwanzo rasmi wa kampeni ya Ukuta. Rais John Magufuli alijibu kuwa hajaribiwi, akasema kuwa wenye kutaka kumjaribu wathubutu.

  Mwanzoni haikuwa tishio, lakini kadiri Septemba Mosi ilipokuwa inakaribia, ndivyo ambavyo hofu ilitanda. Ukweli upo dhahiri kuwa kundi kubwa la Watanzania, liliamini kuwa Ukuta ungezua machafuko.

  Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), likatangaza kuwa Septemba Mosi ingekuwa maadhimisho yao ya kutimiza miaka 52 ya kuzaliwa. Kwamba nao wangeiadhimisha siku yao kwa kufanya usafi.

  Polisi waliahidi kuvunja Ukuta, JWTZ wakasema watazagaa mitaani kufanya usafi, Chadema wakasisitiza kuwa Ukuta ‘ungejengwa’ tu. Watanzania wakajikuta kwenye hofu kubwa.

  Agosti 31, mwaka huu ilipofika, Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitangaza kuahirisha Ukuta mpaka Oktoba 31, mwaka huu. Sababu akasema ni kupisha mazungumzo kati ya viongozi wa dini na Rais Magufuli.

  Waswahili husema “usiku wa deni hauchelewi kukucha”, kutoka Agosti 31 mpaka Septemba 30 ilikuwa kama vile kufumba na kufumbua, mara siku ikawadia. Mbowe akarejea tena kuahirisha Ukuta.

  Hasara za danadana

  Hapa nitangulie kusema kuwa tukio au matukio yoyote ambayo yana ishara ya uvunjifu wa amani sikubaliani nayo. Tanzania ni muhimu kuliko wanasiasa na matakwa yao ya aina yoyote.

   Sioni mahali ambapo Chadema walikusudia kumwaga damu ya Watanzania, ila naona kuwa msimamo wa dola kama ungekutana na shinikizo la chama hicho na Ukuta wao, maana yake hali ingekuwa mbaya.

  Hivyo niliilaani Septemba Mosi, 2016 kwamba haikupaswa kutokea kutokana na vitisho vya Ukuta na vunja ukuta. Hata ahirisho la Oktoba Mosi, sikukubaliana nalo, maana hali ilishakuwa siyo njema kutokana na mivutano ya kisiasa.

  Hata ahirisho la mara ya pili alilolitoa Mbowe Septemba 30 pia nililiunga mkono. Pamoja na uungaji mkono wangu, lakini ukweli ni kuwa Chadema imepoteza alama nyingi kupitia Ukuta.

  Ni vyema kuweka kando furaha yangu na hali halisi. Nimefurahi lakini wanachama na wakereketwa wa Chadema je? Wale walionunua fulana na kutamba kuwa wangeingia barabarani Septemba Mosi na baadaye Oktoba Mosi?

  Je, ni lini tena Chadema wataaminika watakapoandaa operesheni nyingine? Unapofika hapo ndipo unaona kuwa kama chama wamejitengenezea hali ya kutoaminika. Wakereketwa waliopata moto Septemba Mosi mpaka kuingia gharama ya kununua fulana wameshaakisi hali ya ubabaishaji.

  Hofu ambayo Watanzania walikuwa nayo kila walipoifikiria Septemba Mosi mwaka huu, ni hasara kwa Chadema kila upande.

  Watanzania leo wanazungumza kwamba kumbe walikuwa wanaogopa Ukuta bure tu, maana haukuwa Ukuta wa ukweli isipokuwa yalikuwa magirini ya Chadema ili kumtikisatikisa Rais Magufuli. Faida imekuwa zaidi kwa Magufuli kwamba kweli hajaribiwi.

  Hasara kubwa zaidi ni kuwa chama kinapokuwa na wafuasi waaminifu, hujawa na ari ya kuamini kuwa hakuna linaloshindikana. Baada ya maahirisho mawili ya kalenda kuhusu oparesheni ya Ukuta, watu wameshaona kumbe ulikuwa mchezo wa kutishana na anayetishwa hatishiki kweli.

  Chukua somo hili la mfano; yupo mtu alikuwa na tabia ya kuwatisha watu kwamba amevamiwa na majambazi wanataka kumuua. Anapiga kelele, majirani wanakusanyika kisha anawaambia kuwa alikuwa anawatania.

  Alifanya hivyo mara kadhaa mpaka majirani wakazoea, wakajua ni mtu wa utani. Siku moja kweli alivamiwa, alipiga kelele, lakini hakuna jirani ambaye alitokeza. Watu kwenye nyumba zao walinong’ona “huyu naye tumeshamzoea.”

  Baadaye kikafuata kimya, majirani wakajua alichoka kuita na kuamua kunyamaza. Kulipopambazuka wakagundua kuwa ni kweli jirani yao alivamiwa na kuuawa. Wakaambiana “sisi tulidhani utani kama kawaida yake.”

  Utafika wakati Chadema wanaweza kuwa na mkazo katika operesheni watakayoandaa lakini watu watapuuza kama majirani ambavyo waliamini jirani yao anawafanyia mzaha.

  Haipaswi kusahaulika kuwa uahirishaji mara mbili wa Ukuta, umefuata baada ya ahirisho la Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), waliosema wanakwenda kujaa Dodoma ili kulisaidia Jeshi la Polisi, kuuzuia Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliomchagua Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

  Hiyo ndiyo sababu, hata kabla Sepetemba Mosi haijaahirishwa, wapo watu walitabiri mapema kuwa tukio la Ukuta lingefutwa kama ambavyo lile la kuzuia mkutano wa CCM lilivyofutwa. Wakasema Ukuta ni mkwara kama ambavyo tukio la kuzuia mkutano wa CCM lilivyokuwa mkwara.

  Ukiyatazama hayo unaweza kuyaona ni mambo madogo yenye kupita, lakini ni mabaya yenye kushusha hadhi na imani kwa watu. Ipo siku Chadema watasema wanaleta tukio lingine lakini watu hawatajali, wataendelea na shughuli zao kwa imani kuwa ni kawaida yao kutishia.

  Siasa inavyotaka

  Mwongozo kwa vyama vya kisiasa ni kujiepusha na uamuzi ambao unaweza kukifanya chama kionekane kinadandia hoja au kutangaza agenda na kampeni fulani bila kufanya tathmini ya kina.

  Chama cha siasa hakitakiwi kubabaisha, maana kina wafuasi. Hupaswa kutangaza yale ambayo yanamaanishwa. Kama ni Ukuta kweli uonekane ukijengwa. Chama chenye tabia ya kutishia kisha kinatokomea ‘kuingia mitini’, hukosa mashiko kwa watu.

  Siasa hutaka viongozi wa vyama kutumia muda mwingi kutafakari ili kutoa uamuzi ambao hautakuwa wenye kubabaisha. Suala la Ukuta kabla halijatamkwa, lilipaswa kupimwa namna ya kufanikiwa na njia ya kupita. Kuahirishwa mara mbili maana yake Ukuta ulipitishwa bila tathmini nzuri.

  Kosa la kwanza la Ukuta lilifanyika Julai mwaka huu kwa Kamati Kuu ya Chadema kuketi ndani ya muda mfupi na kuamua. Haukutakiwa kuwa uamuzi wa haraka, ulitakiwa kufanyiwa tathmini ya kina.

  Kosa la pili lilifanyika Agosti 31 katika kuahirisha. Mbowe hakutakiwa kusema Oktoba Mosi wangeingia mtaani, ni kipindi kifupi mno. Kosa la tatu ni tangazo la Mbowe Septemba 30 kuhusu kuahirisha Ukuta Oktoba Mosi, maana alikosa hoja za msingi za kuushirikisha umma. Mwisho Chadema kipoteza alama nyingi za heshima, maana kimeonekana kinababaisha.

  Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao www.luqmanmaloto.com

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku