• Breaking News

  Oct 13, 2016

  WAKUU wa Mikoa, Wilaya Waisoma Namba ya Rais Magufuli

  Ni safari ambayo waliiweka katika kalenda yao na wengine wakachukua fedha wakijiandaa kwenda Simiyu.

   Lakini yote hayo yamebaki kama yalivyo, wamebaki wakizisoma  namba za tarehe za kwenye kalenda, lakini hawataruhusiwa kusafiri.

  Waliokuwa wamechukua fedha za matumizi kwa ajili ya safari hiyo, nao watasoma namba hizo kwa kuzihesabu tu fedha hizo, lakini hawatazitumia, wameambiwa wazirudishe na waliozitumia watazilipa.

  Kwa tafsiri ya mtaani ya wimbo maarufu wa CCM, “kuisoma namba” ni kuonja machungu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali.

  Kwa muktadha wa Serikali ya Awamu ya Tano, hatua hizo ni pamoja na kubana matumizi, kupambana na ufisadi, uzembe kazini, kutowajibika na kuzuia ukwepaji kodi.

  Na hivyo ndivyo unavyoweza kuwaelezea viongozi mbalimbali wa Serikali baada ya jana, Rais John Magufuli kufuta safari zao za kuelekea Simiyu kushiriki sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zinazofanyika kesho.

  Baadhi ya viongozi hao walishawasili Bariadi tayari kwa shughuli hiyo inayokwenda sambamba na maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, na hakuna shaka wengine walikuwa safarini na wengine wakikamilisha taratibu za safari.

  Hali akijua hayo, Rais Magufuli amewataka viongozi ambao walishachukua posho za safari kuzirejesha, hali iliyosababisha baadhi yao waliokuwa tayari mjini Bariadi ambako pia kulikuwa na Wiki ya Vijana kulazimika kuondoka jana.

  Agizo la Rais Magufuli linawahusu wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka za Serikali za Mitaa, mameya na wenyeviti wote wa halmashauri za majiji, miji/wilaya na watumishi ambao huambatana na viongozi hao, ambao taarifa ya Ikulu imesema idadi yao hufikia 1,500.

  Lakini, mwenyekiti wa kamati ya mapokezi ya Mkoa wa Simiyu, Protace Magayane alisema walitoa mwaliko kwa wageni 2,500 kuhudhuria sherehe hizo mbili.

  “Tangazo na agizo hili limeibua changamoto ambayo imenilazimisha kuitisha kikao cha  dharura cha kamati kujadili hatua ya kuchukua kuhusu vyumba na hoteli ambazo tayari tuliweka oda,” alisema Magayane ambaye ni ofisa utumishi wa mkoa.

  “Hatuwezi tena kuendelea kuzishikilia hoteli hizo wakati viongozi tuliowatarajia hawatafika na hata wale waliokwishaingia kulazimika kuondoka kutii agizo la mamlaka ya juu.”

  Magayane alisema makatibu tawala wa mikoa, waratibu wa mwenge wa mikoa na wilaya zote nchini walialikwa.

  “Tayari tulishika vyumba kwenye hoteli zote 93 na kupata vitanda 1,904 sawa na asilimia 76 ya mahitaji ya wageni wote waalikwa tuliokuwa tukiwatarajia,” alisema Magayane na kufafanua kuwa asilimia 24 iliyosalia walitarajia kuwatafutia malazi katika wilaya jirani za Bunda, Maswa, Magu na Busega.

  Mwenyekiti huyo wa kamati alisema tayari walishafanya mawasiliano na viongozi kutoka mikoa na wilaya jirani na kuwashauri kufika Bariadi asubuhi ya Oktoba 14, badala ya leo ili kuepuka changamoto ya malazi.

  Agizo la Rais
  Katika hatua iliyotangazwa jana kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Rais ameagiza viongozi waliokuwa wamealikwa kushiriki sherehe hizo, kutohudhuria.

  “Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote walioalikwa kuhudhuria kilele cha sherehe za Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba 2016 katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha za posho na safari kwa ajili hiyo, wazirejeshe,” inasema taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

  “Kwa kuwa sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya muasisi na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka viongozi wa mikoa na wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.”

  Miongoni mwa wakuu wa mikoa waliokuwa tayari Bariadi, ni Meja Jenerali Raphael Muhuga wa Katavi.

  “Kwa nidhamu na kazi yangu ya jeshi, siwezi kuhoji wala kuzungumzia agizo au amri ya Amiri Jeshi Mkuu; ni utekelezaji tu ndiyo unaofuata na ninaondoka muda huu kurejea Katavi,” alisema mwanajeshi huyo mstaafu.

  Mkuu huyo wa mkoa alisema tayari alishawasiliana na idara ya uhasibu kujua ni kiasi gani cha fedha alilipwa kama posho ili arejeshe kutekeleza agizo la Rais.

  Akizungumza na Mwananchi mjini Bariadi muda mfupi baada ya kufungua kongamano la vijana la kujadili ushiriki wa kundi hilo katika maendeleo ya viwanda nchini jana, Waziri wa Nchi, Ofisi Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana, Wazee na Walemavu), Jenista Mhagama aliunga mkono kauli ya Meja Jenerali Muhuga.

  “Agizo la Rais halijadiliwi, bali linatekelezwa mara moja,” alisema. Waziri huyo alisema agizo hilo halina madhara kwa maadhimisho ya Siku ya Nyerere na sherehe za kuzima Mwenge kwa sababu kila kiongozi atashiriki maadhimisho hayo kwa namna tofauti katika eneo lake.

  “Kwa mfano, maadhimisho ya siku ya Uhuru na Ukimwi hayakufanyika katika mtindo wa sherehe kama watu walivyozoea, badala yake yaliadhimishwa kivingine na kwa ufanisi mkubwa, kila mmoja katika eneo lake,” alisema Mhagama.

  Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema agizo hilo ni mwendelezo wa azma ya Rais Magufuli kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

  Rais Magufuli katika uamuzi huo, alisema kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na wilaya zake na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki sherehe hizo kesho.

  Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa hoteli ambazo viongozi wa Serikali walitarajiwa kufikia, walisema waliagizwa kuweka nafasi kwa ajili ya wageni kuanzia Oktoba 8 hadi 14.

  Magayane alisema kamati yake ililazimika kuwaruhusu wamiliki wa hoteli hizo kuendelea na biashara yao kama kawaida kwa kuwapangisha wageni wengine.

  Meneja wa Hoteli ya Sunga Kingdom, Noel Alfayo alisema hoteli yake haijapata madhara kutokana na agizo la Rais kwa sababu uongozi wa mkoa ulimhakikishia kuwa wageni waliopangwa kufikia hotelini hapo, watafika kama ilivyopangwa.

  “Nimeelezwa kuwa wageni watakaofikia hapa ni wa Ikulu ambao hawahusiani na agizo hilo,” alisema Alfayo.

  Hali ni tofauti kwa Hoteli ya Malaika ambako mmoja wa watumishi aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema tayari wameruhusiwa kuuza vyumba ambavyo awali vilizuiwa.

  Hatua hiyo ya Rais Magufuli ni ya kwanza tangu bajeti yake ya kwanza ipitishwe, lakini pia ni mwendelezo wa hatua zake za kufuta sherehe za maadhimisho ya kitaifa kwa lengo la kuokoa gharama.

  Tofauti na sherehe za awali, uamuzi wa sasa unaweza kushangaza wengi kwa kuwa shughuli hiyo, inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilipitishwa kwenye bajeti ya kwanza ya Serikali ya JPM kwa mwaka 2016-2017.

  Sherehe za awali
  Siku chache baada ya kuapishwa, Rais Magufuli alitangaza kuokoa Sh225 milioni zilizochangwa kugharamia hafla ya wabunge na kuagiza zinunue vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

  Rais Magufuli pia alitangaza kufuta sherehe za Uhuru za Desemba 9, 2015 badala yake akaamuru Sh4 bilioni zilizokuwa zimetengwa, zitumike kupanua Barabara ya Morocco-Mwenge jijini Dar es Salaam.

  Pia aliahirisha sherehe za Muungano, Aprili 26 na kuokoa zaidi ya Sh2 bilioni alizoagiza zianzishe upanuzi wa Barabara ya Ghana hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

   Maoni ya wachambuzi
  Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema jambo lolote linalohusu kubana matumizi ni zuri na linapaswa kupongezwa endapo limefanywa kwa nia njema na kulisaidia taifa.

  Alisema haijalishi Rais Magufuli ametoa uamuzi huo lini, lakini jambo la msingi ni kuangalia kama uamuzi huo una faida kwa taifa.

  “Naona uamuzi huo ni mzuri na una manufaa makubwa sana. Tunapaswa kumuunga mkono,” alisema Profesa Mkumbo.

  Alisema kama ni kosa, basi litakuwa limefanywa na wasaidizi wake wa chini ambao walipaswa kumsoma kiongozi wao anataka nini. Wanapaswa kusoma mazingira na kwenda na wakati.

  Rais alisema tangu awali kuwa msimamo wa Serikali yake ni kubana matumizi, hivyo lolote analofanya la kuokoa au kubana matumizi ni jema,” alisema.

  Aliongeza kuwa ni vyema wasaidizi wake kumsoma na kufanya kazi kwa mtindo unaoendana naye.

  “Hili ni suala lisiloingia akilini hasa katika utawala wa Rais Magufuli. Nchi nzima haiwezi kukusanyika Simiyu kuzima Mwenge. Wasaidizi wa Rais walipaswa kuliona hili mapema,” alisema.

  Profesa Mkumbo alisema inavyoonekana dhana ya kubana matumizi ya Rais Magufuli bado haijaingia kwenye mifupa ya watu wake na hivyo anayo kazi kubwa.

  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema licha ya ukweli kuwa uamuzi wa Rais ni mzuri na pesa zitakazookolewa ni nyingi, lakini kwa nini uamuzi utolewe dakika za mwisho, tena na kiongozi mkuu wa nchi.

  Mbunda alisema suala hili linawahusu zaidi wasaidizi wa Rais na huenda likawagombanisha na wananchi kwa kuona hawamsaidii au hawamshauri vizuri.

  “Uamuzi huu unaweza kumpa sifa Rais lakini unateteresha umoja wa kiuongozi kuanzia ngazi ya Rais, wakuu wa mikoa na watendaji wengine ambao wanaonekana hawamsaidii, maana wangekuwa wanamsaidia walipaswa kumshauri tangu mwanzo,” alisema.

  “Wasaidizi wake katika ngazi zote hawajamuelewa Rais na dhana yake ya kubana matumizi. Ugeni huu ni mkubwa na gharama ni kubwa sana, watu 1,500, usafiri na kulipana posho ni gharama kubwa sana, kama ilikuwa inafahamika, basi kuna makosa ya uongozi,” alisema Mbunda.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku