• Breaking News

  Oct 26, 2016

  WAZANZIBARI 40,000 Wafungua kesi Mahakamani Kuupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeingia kwenye jaribio jingine, baada ya Wazanzibari 40,000 kufungua kesi mahakamani kupinga uhalali wake.

  Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) na Rashid Salum Adiy kwa niaba ya wenzake 39,999, katika Masijala ndogo ya mahakama hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam.

  Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Adiy anasema kuwa msingi wa kesi hiyo ni kwamba Muungano huo haukuanzishwa kisheria.

  “Sisi tunadai Muungano huu hauko kwa misingi ya kisheria na kutokana na ushahidi tulionao, uko kisiasa tu na jambo hili linahitaji mfumo na mwenendo wa kisheria kwa kuwa wenye mamlaka ya nchi ni wananchi,” alisema Adiy. 

  Alisema kutokana na nyaraka walizonazo wanapinga hati ya Muungano inayodaiwa ilisainiwa Aprili 22, 1964 na wanapinga uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kuridhia Muungano huo.

  Wanapinga barua ya Mei 6, 1964, iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kuelezea kutambuliwa kwa Muungano huo.

  Pia, wanapinga uhalali wa barua ya Novemba 2, 1964 iliyopelekwa UN ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria iliyopitishwa na Bunge Desemba 10, 1964 ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Adiy na wenzake wanadai kwa kuwa Muungano ni wa kisiasa, ndiyo maana hauwezi kuleta manufaa kwa pande zote mbili hususani uwiano wa kiuchumi na kielimu.

  Baada ya kuwasilisha nyaraka zao wanasubiri kesi hiyo isajiliwe kwa kupewa namba katika Mahakama hiyo na kupangiwa taratibu za usikilizwaji wake.

  Mbali na Wazanzibari 40,000, pia alisema wanayo majina mengine ambayo watayawasilisha mahakamani baadaye, kesi itakapokuwa imeanza

  1 comment:

  1. Njaa mbaya sana kumbe sasa itabidi muwe koloni kama kweli kuna watu wenye akili kama hawa 40k
   Ni kazi ya Maalimu Seifu hiyo njaa tupu watu wanapigania kuungana yeye na kujitenga tu mpaka awe raisi wa Zanzibar kufa raia kama mimi hataki mbona taabu hamuwezi na haitatokea hata usainishe nchi nzima ukiandikiwa NO ni NO mbona huelewi????

   ReplyDelete

  Siasa

  Michezo

  Udaku