• Breaking News

  Nov 20, 2016

  Bilioni 59.5 Kununua Mashine ya Tezi Dume

  Kiasi cha Sh bilioni 59.5 kimeidhinishwa kwa ajili ya kununua vifaa tiba vya kisasa katika hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani hapa, ikiwemo mashine kwa ajili ya matibabu ya tezi dume na upasuaji wake.

  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Alphonce Chandeka alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi.

  Alisema kiasi hicho cha fedha kimeidhinishwa kununua vifaa tiba vya kisasa ili Watanzania wapate huduma zinazostahili na serikali kutoingia gharama za kupelekwa wagonjwa kutibiwa.

  Chandeka alisema kati ya fedha hizo zilizoidhinishwa na serikali Sh. bilioni 16 zimetengwa kwa ajili ya kununua mashine za kisasa katika ukanda wa Jangwa la Sahara za MRI, CT Scan, Digital Xray na mashine nyingine za uchunguzi.

  Aidha alisema kwa sasa wako kwenye mchakato wa kununua mashine kwa ajili ya upasuaji wa tezi dume na fedha kwa ajili ya kununua vifaa hivyo zimeidhinishwa na kwamba hospitali hiyo iko kwenye mchakato wa kuzungumza na kampuni ya Japan ambayo italeta vifaa kwa ajili ya matibabu ya figo na upandikizaji wa figo.

  Akizungumzia ugonjwa wa tezi dume alisema ugonjwa huo umekuwepo kwa miaka mingi huku tatizo kubwa likiwa ni kuziba kwa njia ya mkojo.

  Alisema wagonjwa wengine wa tezi dume hufanyiwa upasuaji na tatizo hilo huisha lakini kuna wale ambao wanakuwa na tezi dume na ugonjwa wa saratani kwa pamoja, hao inabidi kuanzishiwa dozi ya saratani.

  Chandeka alisema hospitali hiyo ni ya serikali ambayo ilizinduliwa Oktoba 23 mwaka jana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambapo ilianzishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kanda ya kati, kusini na magharibi kwa ajili ya kufanya huduma za uchunguzi na tiba.

  “Hospitali imejikita katika kutibu magonjwa ya moyo, figo, saratani na magonjwa ya macho na kutoa huduma za kisasa zaidi na kufanya upasuaji,” alisema na kuongeza kuwa hospitali hiyo itatumika kama kituo cha kuendeleza watumishi wa afya na kitakuwa kituo kamili cha Kanda ya Afrika Mashariki.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku