• Breaking News

  Nov 8, 2016

  Chadema Wampigania Godbless Lema Mahakama Kuu

  Chadema imetua Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Jeshi la Polisi ikitaka mbunge wa jImbo hilo, Godbless Lema apelekwe kortini.

  Chama hicho kinaiomba Mahakama hiyo kuwaamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali na maofisa wanne wa Jeshi la Polisi akiwamo IGP, kumpeleka mahakamani mbunge huyo kwa madai amepitiliza muda wa kisheria wa kushikiliwa mahabusu na jeshi hilo.

  Mbunge huyo machachari wa Chadema amekuwa rumande tangu Jumatano alipokamatwa mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge na kuwa kitendo cha polisi kumshikilia zaidi ya saa 24 ni kinyume cha sheria kwani amekuwa ndani zaidi ya saa 175, hivyo kinamnyima mtuhumiwa haki za kisheria.

  Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi hiyo, Wakili wa Chadema, John Mallya amesema leo itapangiwa jaji wa kuisikiliza na siku ya kuanza.

  “Jambo ninalolifanya muda huu ni kukusanya hati za wito wa kuitwa mahakamani watu watano tuliowashitaki  ambao ni Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (Central),Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya Jinai mkoa (RCO), Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha (RPC), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mwanansheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mshauri mkuu wa kisheria na anatakiwa mahakamani kueleza kwani wanakiuka masharti ya kisheria,”amesema Mallya.

  Amesema anatarajia kesi yao iliyofunguliwa chini ya hati ya dharura itasikilizwa mapema kwa sababu inahusu mtu aliyenyimwa haki ya dhamana, haki ya kutoa maelezo na haki ya kuletwa mahakamani.

  “Tunataka hawa tuliowashitaki kumleta Lema mahakamani na dhamana yake ifanyiwe mchakato Mahakama Kuu na waiambie mahakama kwanini wasichukuliwa hatua za kisheria kwa kukiuka masharti ya kisheria, pia tumeomba gharama zote za hii kesi zilipwe na Serikali,” amesema Mallya.

  1 comment:

  1. Enter your comment...kila siku yeye? Tu.

   ReplyDelete

  Siasa

  Michezo

  Udaku