• Breaking News

  Nov 1, 2016

  Hatimaye Mshambuliaji wa Azam, Farid Mussa Aruhusiwa Kukipiga Hispania

  Hatimaye mshambuliaji wa Azam, Farid Mussa amepata kibali cha kufanya kazi Hispania akiwa na klabu ya Ligi Daraja la Kwanza ya Club Deportivo Tenerife.

  Farid alipata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu hiyo, lakini alikwama kwa muda kutokana na kukosa kibali cha kufanya kazi nchini humo na kuzua mijadala kwa wadau wa soka wakiamini kuwa huenda Azam imembania winga huyo.

  Farid ambaye pia ni winga wa Taifa Stars, anaongeza idadi ya wacheza wa Tanzania wanaokipiga nje.

  Wengine ni Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu ambaye muda si mrefu atakuwa akikipiga nje baada ya kumalizana na TP Mazembe ya DR Congo na Adi Yussuf anayecheza Mansfield Town inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu, England.

  Uongozi wa Azam umeshatuma taarifa ya kuthibitsha kuwa mchezaji huyo amepata kibali rasmi cha kufanya kazi Hispania katika timu ya Deportivo Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

  Hata hivyo, imeelezwa kuwa Farid anakwenda Tenerife kwa makubaliano maalumu ya pande zote mbili ukiwa ni usajili wa mkopo na Azam itanufaika atakaposajiliwa kwingine.


  Ilivyo Club Deportivo Tenerife

  Club Deportivo Tenerife, S.A.D. ni klabu ya soka yenye maskani yake kwenye mji wa Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, katika Visiwa vya Canary nchini Hispania.

  Ilianzishwa mwaka 1912, na kwa sasa inacheza Ligi Daraja la Kwanza inayoitwa Segunda División.

  Timu hiyo hucheza mechi zake Estadio Heliodoro Rodríguez López, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 23,660 waliokaa.


  Changamoto ya Farid

  Farid anakwenda Tenerife iliyoshehemu Wahispania lakini ina wageni kama Anthony Lozano aliyeletwa kwa mkopo kutoka Olimpia ya Honduras sawa na Haythem Jouini (Espérance ya Tunisia) Amath Ndiaye, Msenegal aliyekuwa akichezea Atlético Madrid, kipa raia wa Venezuela, Dani Hernández na Mfaransa, Samuel Camille ambaye ni beki.


  Historia

  Kuanzishwa kwa klabu hiyo, ni matokeo ya klabu mbili katika kisiwa hicho na kutokana na klabu mbili, lakini ubatizo wa jina hili, Club Deportivo Tenerife ulikuwa mwaka 1922. Klabu hiyo ina umri zaidi ya La Liga iliyoanza mwaka 1928.

  Wakati inaanza, timu hiyo ilikuwa ikicheza ligi ya mikoa hadi ilipopanda Segunda División mwaka 1953. Mwaka 1961, ilifikia hatua ya juu zaidi kukaribia kutwaa ubingwa.

  Baada ya miaka 27 ilishuka daraja na ilihangaika kupanda. Katika harakati zake, ilishindwa na kushuka hadi Tercera División ambalo ni daraja la hatua ya tano na sita katika Ligi ya Segunda División B, ni sawa na Daraja la tatu na ilianzishwa mwaka 1978.

  Mwaka 1985, wakati Tenerife ikishuka daraja la tatu kwa mara nyingine, Javier Pérez alichaguliwa kuwa Rais wa klabu. Mwaka uliofuata ikapanda daraja la pili, miaka miwili baadaye ikaja Daraja la Kwanza, baada ya kuishinda Real Betis jumla ya mabao 4–1 katika mechi ya mchujo.

  Jorge Valdano aliichukua timu hiyo mwaka 1991, kama meneja wa timu na raia huyo wa Argentine aliisaidia hata kuilaza Real Madrid na kuifaidisha Barcelona kutwaa ubingwa.

  Katika msimu wa kwanza miaka ya 90, ilikuwa ikipambana isishuke, na ikamaliza ikiwa ya tano na ikafanya vizuri hata kufika 16 bora ya UEFA, kabla ya kufungwa na Juventus 4-2 na kumaliza kazi.

  Mjerumani Jupp Heynckes aliichukua timu kama kocha wake mwaka 1995, na kuiwezesha kumaliza ikiwa ya tano katika msimamo na kuifikisha robo fainali ya Kombe la Hispania.

  Mwaka 1996–97 ilifanya vizuri michuano ya UEFA iliingia nusu fainali kwa kuzitoa Maccabi Tel Aviv, Lazio, Feyenoord na Brøndby (Ilifungwa dakika za nyongeza kwa bao la Antonio Mata), Ubingwa wa Uefa ukaenda kwa Schalke 04.

  Tenerife ilifanya vibaya na mwaka 1999, na hiyo ni kutokana na kuondokewa na makocha na mameneja wake kwenda Valencia; hata hivyo baadaye ilijitutumua na kufanya vizuri mechi za mwisho mwisho za ligi.


  Tenerife ilipotimua kocha

  Pepe Mel alipewa timu kama mkufunzi, Tenerife safari hii ilipata kipigo cha aina yake, ilifungwa mabao 6-0 na Barcelona, na kumfanya kocha huyo atimuliwe. Javier Clemente, mchezaji wa zamani wa Hispania akapewa mikoba, lakini naye hakusaidia kitu, timu ikashuka daraja.

  Tenerife ilikuwa na ukata mkubwa, ilikuwa na madeni yanayofikia Euro40 milioni. Rais Pérez naye akaondolewa na nafasi yake kujazwa na Víctor Perez de Ascanio, ambaye naye alijiuzulu kutokana na utawala mbovu.

  Baada ya Ascanio kuondoka, nafasi yake ikachukuliwa na Miguel Concepción, ambaye aliunganisha timu na wafanyabiashara wakubwa na kuunda kampuni kama sehemu ya klabu. Juni 13, 2009, Tenerife ilirudi La Liga baada ya kuifunga 1–0 Girona. Hata hivyo, ilishindwa kuhimili vishindo, ikafungwa 1-0 na Valencia mechi ya mwisho na ikashuka. 2010–11 ilibadilisha makocha lakini Tenerife haikukwepa kushuka, ikashuka hadi daraja la tatu baada ya miaka 24. Juni 2, 2013, iliongozwa na Álvaro Cervera, ilipanda daraja la pili baada ya kuilaza Hospitalet 3–2 mechi ya mwisho kabla ya Daraja la Kwanza.

  Timu hiyo imekuwa ikipanda na kushuka lakini kwa muda mrefu sasa imebakia Daraja la Kwanza ikipigana kucheza La Liga.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku