• Breaking News

  Nov 24, 2016

  Huu Hapa Ushauri wa Mzee wa Upako Kwenda Kwa Rais Magufuli Kuhusu Wapinzani

  Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lililopo Ubungo-Kibangu jijini Dar, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, amemsihi Rais Dk. John Magufuli kuwa na utayari wa kusikiliza hoja muhimu za wapinzani.

  Mzee wa Upako aliyasema hayo alipozungumza na gazeti hili wiki mbili zilizopita, alipokuwa akitoa maoni yake juu ya mwaka mmoja wa Rais Magufuli.

  Alisema ni vema Rais  Magufuli akawa na utayari wa kusikiliza kelele za wapinzani kwa sababu baadhi yake zina hoja za msingi.

  Mchungaji huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa dini waliopata nafasi ya kutembelewa na Rais Magufuli Kanisani kwake alisema wanachama wenzake wa CCM hawawezi kumpigia kelele kutokana na uoga wa kushughulikiwa kisiasa, hivyo watu pekee wanaoweza kufanya hivyo ni upinzani.

  Hata hivyo pamoja na kumshauri Rais, lakini pia aliwataka wapinzani kuwa na mipaka katika kusema ili kulinda masilahi ya nchi.

  “Ila wapinzani pia waseme kwa mipaka ili kulinda masilahi ya nchi. Kila kitu kizungumzwe kwa wakati wake,” alisema.

  Mbali na ushauri huo, lakini pia Mzee wa Upako alimwagia sifa Rais Magufuli kwa kufanya mambo mengi mazuri ndani ya kipindi chake cha mwaka mmoja ikiwa ni pamoja na kuwataka Watanzania waendelee kumwombea rais huyo kwa kuwa amethubutu kupambana na watu waliozoea kula kwa mikono na miguu bila kunawa.

  Alisema Rais Magufuli amefanikiwa kurudisha nidhamu kwa watumishi wa serikali.

  “Sasa watumishi wa umma wamekuwa na hofu ya kukiuka maadili ya utumishi, hata kama kuna mambo yanafanyika kinyume na sheria ni kwa kificho sana, kwa hiyo mwaka mmoja tumeona mabadiliko makubwa sana, nidhamu imerudi, pili ametimiza baadhi ya ahadi zake kama ile ya kutoa kila mwezi zaidi ya bilioni 28 kwa sekta ya elimu. Pamoja na hayo amehamasisha uchangiaji wa madawati tunaona imetimia, mwaka wa pili haya mengine yatatekelezeka.

  “Pia kwa mwaka mmoja amefunga mianya mingi ya ufisadi, mishahara hewa, wafanyakazi hewa ameokoa mamilioni ya fedha, lakini kitendo cha kuchukua fedha za serikali kutoka benki binafsi na kupeleka Benki Kuu (BOT) ni hatua kubwa kuimariza uchumi na nguvu ya serikali kwa sababu serikali inaweka fedha benki inakopa fedha yake yenyewe inarudisha na riba, pia sheria ya manunuzi ya umma, ameivalia njuga na kuifanya kutokuwa mwanya kwa upotevu wa mapato ya serikali, pia ukusanyaji wa kodi na ukarabati mkubwa wa mwenendo wa bandari ya Dar es salaam, tumeona pia ameimarisha umoja na utulivu aliokuta,” alisema.

  Alisema ingawa si sahihi kumpima kiongozi wa nchi maskini kama Tanzania kwa mwaka mmoja, ni dhahiri kuwa hatumtendei haki kwani ilipaswa kumpa walau miaka minne.

  “Ila kuna mambo tunaweza kusema amethubutu amefanya hayo tunayaona. Namuomba aendelee hivyohivyo na Watanzania tumuombee Mungu ampe nguvu maana kupambana na majitu yaliyozoea kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa si kazi ndogo. Kwa miaka hii mitano tutaona mabadiliko,” alisema.

  Alisema Watanzania wasifedheheke  kutokana na sera za Rais Magufuli za kubana matumizi na kuzuia safari za nje kwa kuwa baada ya muda mfupi hali itakuwa shwari.

  “Watu walikua wamezoea kusafiri ovyo, ilikuwa hakuna sababu ya kuwa na mabalozi nje ya nchi  kwa sababu safari zote walikuwa wanasafiri, lakini kitendo chake cha kufanya shughuli zote za nchi kushughulikiwa na mabalozi wawakilishi ni jambo zuri sana. Sasa watu walikuwa wanahamisha fedha kwenye mikono michafu… ndio wakati wa kuihamisha kutoka kwenye mikono hiyo hivyo watu wavumilie maumivu hiki ni kipindi cha mpito.

  “Namsisitiza Rais akamate hapohapo baadaye fedha itatoka kihalali. Nafuu watu wawe na fedha chache halali ila si haramu, na kimsingi watu wanaosema fedha mtaani hamna ni waongo kwa sababu watu walikuwa hivihivi hamna anayesema alikuwa na fedha nyingi. Zaidi walikuwa wanazitumia hovyo kwenye mahoteli na mabaa.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku