• Breaking News

  Nov 7, 2016

  Magereza Kujaa Waandishi wa Habari, Wasomaji

  Tangu kuanza kazi kwa uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, joto ndani ya tasnia ya habari limekuwa likiongezeka.

  Tasnia hiyo inakabiliwa na vitanzi vya sheria kandamizi, ukatili na unyanyasaji wa waandishi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

  Wapo waandishi waliofanyiwa ukatili kwa kupigwa wakiwa kazini, kupewa vitisho au kujeruhiwa. Pia azimio la kuzuia kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja, kufungiwa kwa magazeti na redio na kuwapo kwa sheria kandamizi.

  Mwaka 1801, miaka ishirini na tano baada ya Marekani kupata uhuru kutoka kwa Uingereza, kijana mdogo Thomas Jefferson alitawazwa kuwa rais wa tatu wa nchi hiyo. Magazeti yalimshambulia sana, na alipambana nayo: “Nalaani uozo unaoenezwa na magazeti…,” alisema na kuongeza: “Tumefika mahali ambapo hatuwezi kuamini chochote kinachoandikwa kwenye magazeti.”

  Pamoja na hayo, Thomas Jefferson aliamini kuna umuhimu wa vyombo vya habari imara na huru. “Kama ingekuwa ni amri yangu kuchagua iwapo tuwe na Serikali bila magazeti ama magazeti bila Serikali,” alisema na kuongeza: “Basi nisingesita hata kidogo kuchagua magazeti bila Serikali.”

  Ni jambo la kawaida kabisa kwa viongozi wa Serikali kuchukia vyombo vya habari. Katika jambo hili, viongozi wetu na wale wa nchi nyingine duniani wanakubaliana. Na zama hizi zinafanana na zama za mwaka 1800 kule Marekani.


  Lakini, mtazamo wa Rais Jefferson ni kwamba bila ya kuwa na vyombo vya habari imara na huru, hakutakuwa na uwajibikaji.

  Nchini Tanzania, Sheria ya Magazeti (1976) ndiyo sheria mama inayoongoza utendaji wa magazeti. Sheria hii imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu kwa kumpa Waziri mamlaka ya kuyafungia magazeti bila taarifa ama kukata rufaa. Sheria hii inatumika mwaka huu tu wakati kuna vyombo vinne vya habari vimefugiwa.

  Mwaka 1992, Tume ya Jaji Francis Nyalali, iliyopendekeza mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, ilieleza kuwa Sheria ya Magazeti hiyo inakuika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu hiyo kuu, ilipaswa kurekebishwa au kufutwa ili kuulinda uhuru wa vyombo vya habari.

  Tume ya Nyalali ilitambua uhuru wa vyombo vya habari una umuhimu wa kipekee katika kustawisha demokrasia na maendeleo ya nchi. Vyombo huru vya habari hufuatilia kazi zinazofanywa na Serikali pamoja na kuwapa nafasi wananchi kuchangia maoni yao kwenye masuala mbalimbali ya jamii na taifa la Tanzania.

  Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari uliopitishwa bungeni wiki iliyopita kwa namna ulivyo, utaudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari.

  “Kuupitisha muswada ule bila kuufanyia marekebisho makubwa na ya msingi ni hatua ya kuihatarisha demokrasia yetu changa,” anasema.


  Mapungufu katika muswada

  Eyakuze anabainisha mapungufu manne katika muswada huo kuwa kwanza kuwa unaipa Serikali mamlaka makubwa ya kuwabana waandishi wa habari. Hususan kwa kuanzisha mfumo utakaowataka kupata vibali kupitia Bodi ya Ithibati ya Wanahabari ambayo itakuwa na wajumbe saba ambao watateuliwa na Waziri.

  Sheria na taratibu za kimataifa zipo wazi, si halali kutoa vibali kwa waandishi wa habari ama kuweka masharti ya nani anaweza kuwa mwandishi wa habari. Muswada huu ukipitishwa kuwa sheria, waandishi wote wa habari nchini watajazwa na hofu yakufanya kazi zao ipasavyo kwa kuogopa kunyang’anywa vibali vyao.

  Pili, muswada unataka vyombo vya habari (magazeti) kuwa na leseni. Unaipa Serikali mamlaka ya kusimamia utoaji wa leseni hizo. Tatizo kuu la Sheria ya Magazeti (1976) litaendelea kubaki palepale.

  Tatu, muswada uniingilia uhuru wa vyombo vya habari kwa kuweka uwezekano wa kuvilazimisha vyombo vya habari vikiwamo vya binafsi kutangaza habari kama inavyoelekezwa na Serikali.

  Nne, vifungu vya muswada vinavyohusika na kauli za kashfa na uchochezi vinavuka mipaka inayokubalika kwenye nchi za kidemokrasia. Kifungu kimoja kwa mfano kinasema kauli iliyochapishwa inaweza kusemekana kuwa ni ya kashfa hata kama ni ya ukweli. “Muswada wa sasa unaainisha kuwa kauli ni lazima iwe ya kweli na “yenye manufaa kwa umma”. Na bila shaka Serikali ndiyo itakayoamua kauli ipi ina manufaa kwa umma,” anaeleza Eyakuze na kuongeza:

  “Hakuna mtu anayedai kwamba vyombo vya habari hapa Tanzania vimekamilika kimaadili na kitaaluma. Tasnia ya habari nchini inaandamwa na matatizo ya upendeleo, usahihi wa habari, rushwa na uongo wa kupindukia. Kuna utofauti kubwa kati ya Marekani ya mwaka 1801 na Tanzania ya mwaka 2016, lakini malalamiko mengi ya Thomas Jefferson kuhusu magazeti ya Marekani miaka 200 iliyopita yana uhalisia hapa nchini Tanzania.

  “Lakini, jawabu la Jefferson halikuwa kutunga sheria zenye lengo la kuubana uhuru wa magazeti yaliyomkera. Hili linapaswa pia kuepukwa nchini Tanzania. Vyombo huru vya habari na vinavyojitegemea ni sehemu muhimu ya serikali ya kidemokrasia inayowajibika.”

  Anasema muswada huo ukisainiwa kuwa sheria, utaunyonga uhuru wa vyombo vya habari nchini na kusababisha janga kubwa la uwapo wa Serikali isiyokuwa na magazeti.

  Wadau chini ya kivuli cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), walipendekeza muswada huo upelekwe bungeni Februari mwaka 2017 badala ya Bunge la Novemba kwa kuwa una kasoro nyingi ambazo zinatakiwa kujadiliwa na wadau wote kwani takriban asilimia 70 ya waandishi walengwa wako mikoani.

  Mwenyekiti wa zamani wa TEF, Absalom Kibanda alisema wazi mbele ya kikao cha uchambuzi wa kifungu kwa kifungu katika muswada kwamba tasnia ya habari kwa sasa inatazamwa kama biashara ya ujangili nchini.

  Kibanda anasema kuanzia kifungu cha kwanza hadi cha mwisho cha sheria hiyo vimeandikwa kwa hali ya ukatili.

  Hoja na utetezi wa Serikali

  Waziri mwenye dhamana ya habari, Nape Nnauye alitumia muda mwingi kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika mitandao ya kijamii kuhusu muswada huo huku akitofautiana kauli na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

  Msemaji wa Serikali, Hassan Abbas anasema kuhusu adhabu hata mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) umeweka wajibu licha ya kueleza uhuru wa habari katika ibara ya 19, lazima wanahabari kulinda hadhi ya watu wengine, kulinda usalama wa taifa na masuala ya maadili..

  Abbas ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) anasema Serikali inayo nia njema kwa tasnia hiyo iliyosahaulika kwa miaka 20 bila kutambuliwa kisheria.

  Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya habari wa Maelezo inaeleza sababu tano za kukubaliana na muswada huo. Kwanza; ni heshima ya tasnia kwa kupunguza waandishi waliokosa taaluma na weledi (makanjanja).

  Pili; ni kudhibiti kila aliyeweza kujitengenezea blogu yake kwa ajili ya habari.

  Tatu; ni msisitizo wa elimu kutokana na tatizo la watu kupita njia za mkato kuingia katika fani hiyo na kutokuwa tayari kwenda shule kusoma.

  Katika Ibara ya 21, muswada huu unazungumzia mfuko wa mafunzo ya habari wenye malengo matatu ikiwamo kuwezesha mafunzo kwa wanataaluma ya habari, kukuza programu za uendelezaji wa maudhui ya ndani ya nchi. Kwa mujibu wa Ibara ya 22, mfuko huo, utapata fedha kutoka bungeni, misaada na zawadi na michango ya vyombo vya habari.

  Sababu nyingine ni umuhimu wa Baraza Huru la Habari ambalo kila mwanahabari aliyethibitishwa atakuwa mwanachama wa baraza hili. Ibara ya 25 (1) inaeleza kazi za baraza hili kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati zitakuwa ni kuandaa na kuidhinisha kanuni za maadili ya taaluma ya habari na kukuza maadili na viwango vya taaluma vya wanahabari na kampuni za habari.

  Sheria hiyo itasaidia kulinda masilahi ya waandishi wa habari wanapopata majanga wakiwa kazini, maradhi, kustaafu au kuachishwa kazi. Kila mwajiri atatakiwa kuweka bima na hifadhi ya jamii kwa kila aliyeajiriwa katika chombo cha habari husika na wanahabari wa kujitegemea watapaswa kujiwekea kinga kwa mujibu wa sheria hiyo.

  Pia, sheria hiyo inatoa mwelekeo wa vyombo vya habari kuhusu jinsi ya kufanya kazi kwa ufanisi, kuzingatia maadili na weledi. Katika hili, sheria imeeleza majukumu ya vyombo vya habari vya umma na binafsi ili kuhakikisha yanaleta tija kwa taifa.

  Pamoja na fursa hizo, Mwakilishi kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike anakiri ni kweli hakuna uhuru uliopitiliza, lakini hofu iliyopo ni kuwa adhabu zilizotajwa katika muswada huo zinatafsiriwa kama mpango wa kupunguza makali ya mwandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yake.

  Madudu ya muswada

  Pamoja na hoja hizo, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile anataja baadhi ya vifungu hatari katika muswada huo ambavyo vinatakiwa kuondolewa.

  Anasema kifungu (60) kinachompatia mamlaka Waziri mwenye dhamana kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya sheria hiyo; kifungu cha (55) kinachompatia mamlaka Waziri kuzuia uchapishaji na utangazaji wa maudhui yanayohatarisha usalama wa taifa au afya ya jamii.

  Kifungu cha 52 kinachoagiza utoaji wa faini ya isiyopungua Sh15 milioni kwa kila mtu atakayehusika katika kosa lolote litakalotendwa na kampuni, shirika, kikundi, umoja au chama.

  Kifungu cha 50(2) kinasema mtu yeyote bila kuwa na sababu inayokubalika kisheria kama atakuwa na chapisho linalochochea uasi, atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia kwa kosa la kwanza, atalipa faini isiyopungua Sh2 milioni na isiyozidi Sh5 milioni.

  “Vifungu hivyo ni hatari na tunapendekeza viondolewe vyote, vifungu hivyo ni katili sana kwa mwandishi wa habari vinginevyo magereza yatajaa waandishi wa habari na wasomaji,” anasema Balile.

  By Kelvin Matandiko, Mwananchi

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku