• Breaking News

  Nov 7, 2016

  Mdahalo: Trump Atakuwa Bora kwa Tanzania na Afrika Kuliko Clinton?

  Swali hili haliepukiki. Wakati Wamarekani wanajiuliza ni nani anawafaa kuwa Rais wao kati ya wagombea hawa wawili hapo kesho, Watanzania nao kama wananchi wengine duniani – japo hawapigi kura yoyote huko Marekani – wanajiuliza au wanapaswa kujiuliza kabla ya kuamua kumshangilia au kumzomea nani kati ya wagombea wa Marekani – ni nani ataweza kuendana na mwelekeo na mtazamo wa kiuongozi ambao utaleta manufaa kwa Tanzania na labda kwa Afrika nzima.

  Wakati Wamarekani na dunia inasubiria kuona ni nani ataibuka kidedea katika Uchaguzi Mkuu wa Urais Marekani hapo kesho Tanzania na Watanzania nao watakuwa wanaangalia uchaguzi huo kwa macho ya tofauti kidogo kuliko ilivyokuwa miaka kama nane iliyopita wakati Rais Obama amechaguliwa kwa mara ya kwanza. Katika uchaguzi ule wa 2008 Tanzania na labda Waafrika wengi walitarajia kuwa ujio wa Rais mwenye asili ya Afrika unaweza kuja na matokeo ya tofauti sana na bora zaidi kwa bara la Afrika labda kuliko marais wengine wote waliowahi kupita huko Marekani, taifa lenye nguvu zaidi ya kiuchumi na kijeshi duniani.

  Nchini Marekani watu weusi wanatarajiwa na wakati mwingine wanadhaniwa kuwa wanaunga mkono chama cha Democrat kwa sababu tu ya rangi yao. Ilikuwa ni jambo la ajabu kumkuta mtu mweusi mwaka 2008 ambaye alikuwa hamuungi mkono Obama; kwani ilidhaniwa kwa vile ni ‘mweusi mwenzake’ basi atamuunga mkono hata kama hajui au hajali sera zake mbalimbali. Jambo hili hata hivyo halidhaniwi kwa watu weupe. Kwa mfano, leo hii katika kampeni hii ukikutana na mwanamke mweupe huwezi kumdhania kuwa anamuunga mkono Hillary Clinton (mwanamke mweupe mwenzake) kwa sababu kumdhania hivyo ni kuonesha kutokumjali huyo mtu na uwezo wake wa kufuatilia mambo ya kisiasa. Ni kwa sababu hiyo hakuna mtu anayeshangaa kuona meneja wa kampeni ya Trump ni mwanamke na kuwa amezungukwa na anashangiliwa na wanawake wengi weupe pote Marekani.

  Kuungwa mkono kwa Obama kwa sababu ya rangi yake kulifanyika hata Tanzania na miongoni mwa Watanzania. Wapo ambao walimuunga mkono kwa sababu ya sera zake na za chama chake lakini wapo wengi ambao walimuunga mkono kwa sababu tu alikuwa ni “mweusi mwenzao”. Lakini wapo wengine walimuunga mkono kwa sababu anatoka chama cha Democrat ambacho kinadhaniwa kuwa ndicho kinacholinda maslahi ya watu weusi huko Marekani.

  Watu wengi kwa mfano ambao wanamchukia Rais aliyemtangulia Obama – George W. Bush – wanamchukia kwa sababu alikuwa na sera ambazo zilileta migogoro mingi Mashariki ya kati na uvamizi kama wa Iraq ulimjengea sifa na kuimarisha sifa ya chama cha Republican kuwa ni chama cha ubabe na kupinga ukandamizaji. Kwa Watanzania na Waafrika wapo watu wengi ambao wanaamini kabisa kuwa Rais Bush alikuwa ni mbaya sana kiasi kwamba wako tayari kukubali karibu mambo yale yale yakifanywa na Obama kwa vile ni mweusi lakini wangepiga kelele sana kama yangefanywa na Rais mweupe.

  Hata kama ni kweli kuwa kati ya Obama na Bush ni Bush ambaye ameacha matokeo bora zaidi na kuokoa maisha mengi ya Waafrika kuliko Obama alivyofanya. Mpango wa PEPFAR wa Rais Bush ambao uliwezesha upatikanaji wa dawa na huduma mbalimbali kwa watu waishio na VVU uliweza kuokoa maisha ya watu wengi katika Bara la Afrika kuliko ambavyo ingetokea kama mpango huo usingekuwepo. Hata hivyo, Obama na mipango yake ya kuleta uwekezaji na biashara kupitia US-Africa Business Forum (USABF) na ule wa Power Africa (kueneza nishati ya umeme vinaweza kutajwa kuwa kuwa ndio mafanikio yake makubwa zaidi ya kisera katika Afrika japo mipango hiyo haijakamilisha matokeo yake yote.

  Hili linatuleta kwenye uchaguzi wa hapo kesho. Je, viongozi hawa wawilil wana mpango au maono gani na Bara la Afrika? Je, ni nani kati yao ambaye sera zake kwa bara zetu zitakuwa na matokeo mazuri kwa Tanzania na bara zima?

  Na. M. M. Mwanakijiji
  Kutoka ZamaMpya.com

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku