• Breaking News

  Nov 3, 2016

  Mwamuzi wa Mbeya City Vs Yanga Jana Alikuwa Sahihi: Kamati

  Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania imesema kuwa maamuzi yaliyofanywa na mwamuzi wa mchezo kati ya Mbeya City na Yanga siku ya jana katika dimba la Sokoine Mbeya, yalikuwa sahihi kwa asilimia 100.

  Mwenyekiti wa kamati hiyo, bwana Salum Umande amesema kitendo cha mwamuzi wa mchezo ule kukubali bao la pili la Mbeya City, kilikuwa ni sahihi kwa mujibu wa kanuni za uchezeshaji na kwamba haoni tatizo lolote katika bao lile licha ya kulalamikiwa na wachezaji wa Yanga.

  Umande pia ametetea kitendo cha mwamuzi huyo kubadili maamuzi yake mara mbili, na kusema kuwa kilichotokea ni hofu ya kawaida ya kibinadamu baada ya kuzongwa na wachezaji wa Yanga.

  "Mwamuzi yule alichezesha vizuri na maamuzi yake yalikuwa safi kabisa, mimi sioni tatizo lolote, lile bao lilikuwa ni bao halali lakini alipozongwa na wachezaji wa Yanga aliogopa tu, lakini baadaye alitafakari akaona maamuzi yake ya awali yalikuwa sahihi na ndiyo maana akabadili tena maamuzi na kuhesabu kuwa ni bao"

  Kuhusu mwenendo wa waamuzi katika msimu huu wa ligi, Umande amesema hadi sasa hajaona matatizo makubwa zaidi ya mapungufu ya kibinadamu, na kuongeza kuwa kamati hiyo ina mpango wa kufanya mapitio ya kazi za waamuzi wote wa ligi kuu mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ili kuwaondoa waamuzi watakaoonekana wamefanya vibaya.

  "Mzunguko wa kwanza ukimalizika tutaangalia nani hafai, tutamuondoa, na kuwaweka wengine, nchi hii haina tatizo la waamuzi, tuna waamuzi zaidi ya 300 lakini walichaguliwa kuchezesha ligi ni 24 pekee" Amesema Umande.


  Kwa upande wake mchambuzi wa michezo kutoka EATV na EA Radio Tigana Lukinja akizungumzia bao la pili la Mbeya City amesema kwa mujibu wa kanuni, mpira wa kutengwa katika maeneo ya karibu na 18 kama ilivyokuwa jana, timu pinzani inapaswa kuweka ukuta miguu kumi toka mpira ulipotengwa kitendo ambacho kinapaswa kuhakikiwa na mwamuzi kabla ya kuruhusu mpira huo wa adhabu kupigwa.

  Tigana amesema katika hali kama ile Mbeya City hawakupaswa kupiga mpira ule bila ruhusa ya mwamuzi ingawa Yanga pia walipaswa kuzuia mapema "Angalau mchezaji mmoja wa Yanga alipaswa kukaa mbele ya mpira ili hadi mwamuzi amtoe, sasa kama wao hawakufanya hivyo na kwa kuangalia uzoefu wao kimataifa, wanapaswa kujilaumu kwa hilo na hasa benchi lao la ufundi kwa kutowafundisha jambo hilo" Amesema Tigana na kuhitimisha kuwa katika mazingira kama hayo hilo ni bao halali.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku