• Breaking News

  Nov 25, 2016

  Sinema Mpya Sakata la Polisi Wanne Kumvua Nguo Mchungaji


  Moshi. Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti tukio la polisi wanne wanaodaiwa kumvua nguo mchungaji wa kanisa moja nchini akiwa na mtu mwingine na kumhusisha na vitendo vya ushoga kisha kumdai Sh10 milioni ili kulimaliza, shuhuda mmoja amejitokeza na kusimulia mkasa mzima.

  Katika tukio hilo la Novemba 18, mchungaji huyo anadaiwa kufanyiwa kitendo hicho baada ya kukaribishwa katika nyumba moja ya wageni huko Bomang’ombe, Hai na mtu mmoja waliyekuwa na miadi ya kibiashara ambaye alitaka ajue mahali alikofikia.

  Shuhuda huyo, mmoja wa wahudumu katika nyumba hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema mtu huyo ndiye aliyewaita polisi alipotoka na kumwacha mchungaji chumbani na kabla ya kuwapigia simu askari hao, aliagiza chai kwenye mgahawa huo.

  “Alikuwa akiwahimiza polisi wafanye haraka kabla hajarudi chumbani. Wale polisi walipokuja akawaambia wasubiri dakika chache ndipo wamfuate chumbani. Yeye akarudi chumbani lakini kiukweli hawakuwa wamefanya hicho kitendo (ushoga),” alisema.

  Alisema aliwasihi polisi wasiwatoe watu hao muda huo (saa kumi na moja alasiri) akisema kufanya hivyo kungeweza kuharibu jina la hoteli yao.

  Polisi, Takukuru wamsaka


  Akizungumzia sakata hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema jana kwamba wako njiapanda kwa vile maelezo ya mchungaji huyo kwa Takukuru yanatofautiana na yale aliyoyatoa polisi.

  “Wakati akisimulia huo mkasa kule Takukuru mimi nilikuwepo na ndiyo haya yaliyopo kwenye gazeti (Mwananchi) lenu la leo (jana) lakini cha ajabu maelezo aliyoyatoa polisi ni tofauti kabisa,” alisema. “Hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa tunamtafuta kwa sababu yeye siyo mtuhumiwa lakini tungependa aje atueleze utofauti huu wa hadithi yake.”

  Kamanda wa Takukuru Mkoa Kilimanjaro, Alex Kuhanda alisema jana kuwa, “Sisi ndiyo tuliompokea na kumsikiliza na baadaye tukawakabidhi wenzetu wa polisi lakini tangu Jumamosi (Novemba 19), hatumpati kwenye simu ili atupe mrejesho,” alisema Kuhanda licha ya kuahidi kufika katika ofisi hizo kwa ajili hiyo.

  Ilivyokuwa

  Mchungaji huyo anadaiwa kukutana na dereva wa malori eneo la Njiapanda ya Himo na kuweka miadi ya kuwasiliana kwa ajili ya biashara ya pumba hivyo walipeana namba za simu ili zikipatikana apigiwe.

  Siku iliyofuata mtu huyo alimpigia akisema amepata magunia 150 na kumtaka mchungaji afike Bomang’ombe kuziona pumba hizo. Alipofika, kabla ya kwenda kuziona, alimuomba mchungaji amsindikize ili achukue chumba kwani siku hiyo angelala hapo kusubiri wenzake kutoka Segera.

  Walifuatana na baada ya kupewa funguo, alimtaka mchungaji aingie kukiona kabla ya kumwambia amsubiri hapo akanunue sigara ili akirudi waende kuangalia na aliporudi tu, ndipo walipoingia na watu wengine ambao baadaye wanne walibainika kuwa polisi na kuwalazimisha mchungaji na mtu huyo kuvua nguo, na kuwarekodi kwa picha wakiwatuhumu kufanya ushoga.

  Ilidaiwa kwamba waliwachukua wakiwa nusu uchi hadi kituo cha Polisi cha Bomang’ombe na kutaka wapewe Sh10 milioni ambazo hata hivyo hazikupatikana na badala yake wakapewa Sh5.4 milioni.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku