• Breaking News

  Nov 29, 2016

  Tazara Yasubiri Utekelezaji wa Mazungumzo ya Marais Magufuli na Lungu

  Huenda Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ikafanya vizuri katika siku za usoni baada ya makubaliano kufikiwa kati ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu na John Magufuli.

  Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kubadilisha sheria iliyoliunda shirika hilo ili kuliwezesha kupata watendaji wanaoweza kuliendesha kibiashara.

  Msimamo huo umetolewa Ikulu ya Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu Rais Lungu kuwasili nchini juzi kwa ziara ya siku tatu.

  Tazara ilizinduliwa mwaka 1976 baada ya kujengwa kwa miaka minne na Serikali ya China kwa lengo la kuziwezesha Tanzania na Zambia kusafirisha mizigo. Zambia, ambayo haipakani na bahari inahitaji usafiri huo kwa ajili ya kusafirisha shaba baada ya kushindwa kutumia Bandari ya Durban, Afrika Kusini iliyokuwa imefungiwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na siasa za kibaguzi wakati huo.

  Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Rais Lungu amekiri kuwepo kwa hali mbaya ya kibiashara ndani ya Tazara akisema ni kutokana na uongozi ubovu.

   “Katika mazungumzo na Rais Magufuli, tumekubaliana kwamba usimamizi mbovu ndiyo umekuwa tatizo uliyoiangusha Tazara. Kama tunaweza kuboresha uongozi tunaweza kuifufua. Tunajua gharama kubwa iliyotumika kujenga reli ile na kazi kubwa iliyofanywa na watu wetu, watu wa China waliojenga,” amesema Lungu.

  Rais Magufuli amesema Tazara ilipoanzishwa ilikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni tano lakini mwaka 2005 uwezo huo ukashuka hadi kufikia tani 500,000 na kwa sasa Tazara inaweza kubeba tani 128,000 tu kwa mwaka.

  “Ukizungumza na uongozi wa Tazara watakwambia kuna tatizo la mtaji, lakini ukweli tatizo ni uongozi. Kwa sababu kama ni mtaji walikuwa nao tangu mwaka 1976. Lakini mtaji sasa umeshuka mpaka hapo. Tumekuwa pia tukisikia matatizo ya Tazara hata katika kulipa mishahara ya wafanyakazi,” amesema Rais Magufuli.


  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku