• Breaking News

  Nov 13, 2016

  Uchambuzi:Namna Ambavyo Mkataba wa EPA Ungeliangamiza Taifa

  Wakati  wabunge wamemsihi Rais John Mafuguli kutotia saini mkataba wa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA), Imebainika kuwa Tanzania ingepoteza dola milioni 984 (zaidi ya Sh. trilioni mbili) kwa mwaka kutokana na kuingia kwa bidhaa kutoka kwenye nchi hizo ambazo hazitalipiwa kodi.

  Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabatho Nyamsenda, aliyasema hayo juzi mjini Babati, Manyara kwenye mkutano wa tisa wa Mtandao wa Wakulima Tanzania (Mviwata).

  Nyamsenda alisema athari ya kupoteza mapato hayo kwa taifa ni kubwa na awali, Rais Magufuli alishaonyesha njia kwa kukataa kutia saini makubaliano hayo na pia wabunge walipoukataa imekuwa jambo jema. Alisema takwimu zilizotolewa kuwa nchi itapoteza dola milioni 32 (Sh. bilioni 64) kwa mwaka si sahihi kwa kuwa ni takwimu za miaka iliyopita.

  Alisema taasisi ya South Centre ilianzishwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa ajili ya kupigania ushirikiano wa nchi za kusini, zinaeleza kuwa fedha hizo zitapotezwa kutokana na ushuru wa bidhaa ambazo hazitalipwa baada ya mkataba wa EPA.

   Aidha, nchi ambazo zilikuwa zinatozwa mapato nchini hazitatozwa tena na nchi zingine zitashindwa kushindana kwenye soko kutokana na bidhaa za Umoja wa Ulaya, zinazozalishwa kwa unafuu na pia hazitalipishwa kodi.

  “Kutokana na mkataba huo, kutakuwa na upotevu mkubwa wa mapato na pia viwanda vya ndani vitakufa kwani havitaweza kushindana kwenye soko na bidhaa hizo kutoka kwenye nchi za Ulaya,” alisema.

  Endapo nchi ikiingia makubaliano hayo, itasalimisha ushuru, ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuendelea kufanya kazi ya utumwa, kwa kuwa viongozi wa nchi za Ulaya wanataka tuendelee kuwa wazalishaji wa malighafi kwenye soko lao.

  “Tutaendelea kuzalisha mali ghafi za pamba, kahawa na mazao mengine na kupeleka Ulaya kisha wao wanazalisha nguo wanazivaa na kutuletea mitumba na kuja kutuuzia sisi bila wao kulipia ushuru wa kuingiza bidhaa,” alisema.

  Nchi kama nchi haitakuwa na viwanda vya ndani kwa kuwa itashindwa kuvilinda na kuhakikisha unajiwekea ukomo wa aina ya bidhaa zinazoingia nchini na kwa hali hii tutapoteza dhana ya uchumi wa viwanda.

  “Wakulima, wafugaji na wazalishaji wa chini wataendelea kufanya kazi za hali ya chini kwa kuendelea kuchuma pamba, kuchunga mifugo na kurudishwa kwenye hali ya utumwa kupitia makubaliano ya EPA,” alisema.

  Mratibu wa Mviwata wa Mkoa wa Manyara, Martin Pius, aliipongeza serikali kwa kutotia saini mkataba huo kwa sababu makubaliano hayo yanagusa maendeleo ya jumla ya wananchi wa Tanzania hasa wakulima wadogo.

  Alisema wakulima wa Ulaya wanapatiwa ruzuku kwa ajili ya uzalishaji na masoko tofauti na wakulima wa Tanzania, hivyo mkataba huo utakuwa unaumiza kwa kuwa bidhaa zao zitakuwa na bei ndogo tofauti na bidhaa za wakulima wa Tanzania.

   – Nipashe

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku