• Breaking News

  Nov 3, 2016

  VIDEO: Mbunge Bashe Asema, Mipango ya Uchumi ya Serikali ni Mibovu na Hali Mtaani Mbaya Hakuna Pesa

  Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), wamesema uchumi wa nchi unayumba, huku mawaziri walioteuliwa na Rais Dk. John Magufuli wanaogopa kumweleza ukweli kiongozi huyo kuhusu hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi.

  Kutokana na hali hiyo, wamesema ipo haja kwa Serikali kujitafakari na mipango yake mingi ambayo imekuwa na ugumu katika utekelezaji wake.

  Akichangia hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Bajeti, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango bungeni jana, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema hotuba ya waziri huyo haina jipya ila imerudia mambo yaliyopita ya mwaka 2015/16, huku akihisi nchi hii ni ya watu wa hali ya juu pekee.

  Alisema kuwa Waziri Mpango alitakiwa kuichambua ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) Oktoba 20, mwaka huu ambayo inaonyesha uchumi wa nchi umezidi kuporomoka hadi kushika namba 139 duniani.

  Bashe alisema kilichowasilishwa na Waziri Mpango ni tofauti na hali halisi ya maisha ya kawaida ya wananchi waliopo mitaani.

  “Waziri wa Fedha usirudie uliyoyafanya 2016/17, nalisema kwa sababu angalia vitabu vyake hapo, nchi hii si ya Executive Only (si ya watu wakubwa pekee). Unakuja na kitu kilekile, eti eneo la kimkakati Kurasini, huku unataka kuua Kariakoo ili Wachina watumie ile nafasi.

  “Jamani hatuwezi kwenda hivyo, boresheni Kariakoo ili mruhusu hawa waswahili walipe kodi, tuacheni kabisa dhana mbaya.

  “…Sijui kwa kuwa wewe hukuomba kura na hujui hali ngumu iliyopo mitaani, vijijini fedha hakuna halafu unakuja hapa kusema tunatekeleza. Waziri wa Fedha asipochukua tunayomshauri, tuna jukumu la kuungana bila kujali itikadi zetu humu ndani bungeni,” alisema Bashe.

  Alisema ni lazima waziri aangalie sheria za nchi kama zinavutia wawekezaji wote na si wa nje peke yao.

  “Ninashangaa sana katika taarifa ya waziri, anasema mazingira na hali ya hewa itakuwa nzuri huku taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinasema kuna ukame. Leo hali ya hewa kwa nchi jirani unasema ni nzuri si kweli, kwa 2017/18 nchi zinazotuzunguka zina hali mbaya ya chakula na hata taarifa ya TMA inasema hivyo,” alisema

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku