• Breaking News

  Nov 8, 2016

  Wanandoto ya Kala Yafanikisha Kupatikana Kwa Mtoto Aliyepotea miezi 14 iliyopita

  Video ya wimbo ‘Wanandoto’ ya msanii wa muziki wakufoka, Kala Jeremiah imefanikisha kurejesha furaha ya familia moja ambayo ilipotelewa na mtoto wao wa kiume toka September 2015.

  Mama wa mtoto huyo aitwae Adam, alifanikiwa kumuona mwanae huyo kupitia video ya wimbo huo ambao unazungumzia mazingira magumu wanayopitia watoto yatima.

  Akiongea na Bongo5 Jumanne hii, Kala amesema alipigiwa simu na mama huyo akimuulizi mtoto huyo alimuona kupitia video yake ya Wanandoto.

  “⁠⁠⁠Nilipigiwa simu na mtu akaniambia Kuna mama kamuona mtoto wake kwenye video yangu ya Wanandoto na mtoto huyo alipotea tokea mwaka jana mwezi wa 9,” alisema Kala “Mama wa mtoto alifanya jitihada zote za kumpata mtoto wake bila mafanikio lakini juzi juzi akiwa anatazama video ya Wanandoto akamuona mwanae kwenye video na kupata mshangao na mshituko ndipo alipoamua kumtafuta mtangazaji flani wa redio flani ndipo mtangazaji huyo akanitafuta na kuniunganisha na mama huyo,”

  Alilifanua zaidi “Mama yule alinieleza kwa masikitiko makubwa sana kuwa mtoto wake alipotea toka mwaka jana mwezi wa 9 alimtafuta Sana kila sehemu alienda kwa waganga wengi alienda kwenye maombi ya kila aina lakini hakufanikiwa kumpata mwanae.
  adam


  Mtoto Adamu akiwa na mama yake

  Rapa huyo amesema baada ya kumsikiliza mama huyo aliamua kumwelekeza katika kituo cha watoto yatiba ambacho kinamlea mtoto huyo.

  “Baada ya mama huyo kunieleza yote hayo nikawasiliana na kituo cha kulelea watoto cha Chakuwama ambapo mtoto Adam analelewa nikawaeleza habari hii wakakiri kweli Adam yupo na ni kweli walimpata mwaka jana mwezi wa 9. Basi nikawasiliana tena na mama yake Adam na kumwambia kuwa nimewasiliana na mlezi wa kituo amekiri kuwepo kwa Adam kituoni hapo na kwakuwa mimi sipo Dar kwa muda huu nikamuunganisha mama Adam na mlezi wa kituo kile wakawasiliana na jana mama Adam amefika kituoni pale na kuonana na mwanae na amefurahi Sana,”

  Kwa upande wa mama Adam, amemshukuru Kala kwa kufanikisha kupatikana kwa mtoto wake.

  “Kwa kweli namshukuru Mungu kwa kufanikiwa kunionyesha mtoto wangu ana mwaka mmoja na miezi miwili toka apotee na nilitoa taarifa kila sehemu na nikashindwa kumpata. Kwa hiyo naweza kusema video Kala imerudisha furaha yangu, namshukuru sana,” alisema Mama Adam.

  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku