• Breaking News

  Dec 1, 2016

  MSAJILI Amaliza Mzizi wa Fitina

  Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ameeleza sakata la watumishi wa umma kuweka fedha kwenye akaunti ya muda maalumu (fixed deposit accounts), akisema si rahisi kwao kuiba fedha hizo kwa sababu miamala ya benki ni ya uwazi.

  Kauli yake inatofautiana na maelezo ya Rais John Magufuli kuhusu uamuzi wake wa kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), aliposema kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na chombo hicho kuidhinisha uamuzi wa TRA kuweka fedha kwenye akaunti za muda maalumu kwa lengo la kujinufaisha binafsi.

  Aliisema alivunja kwa ‘kosa’ hilo na kurudisha Sh26 bilioni zilizokuwa zimehifadhiwa huko kwa ajili ya kujizalisha kwa njia ya riba.

  Wakati ikitofautiana na Rais, kauli hiyo inafanana na ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ambaye hivi karibuni alikaririwa akisema kuweka fedha kwenye akaunti hiyo si kosa kisheria.

  Profesa Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa bodi iliyovunjwa ya TRA, alisema hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti ya muda maalumu.

  Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mafuru alisema kwa uzoefu wake katika sekta ya benki, wizi wa fedha zinazowekwa kwenye akaunti maalumu za muda, hauwezekani na kwa sasa hizo ni tuhuma tu, hivyo Serikali imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza.


  Lakini alisema tatizo ni kuweka fedha kwenye akaunti hizo, wakati zinahitajiwa sehemu nyingine kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

  “Nimefanya kazi kwenye taasisi za benki karibu miaka 20 na nimekuwa nikipata wateja wanaofungua ‘fixed deposit account’ zikiwemo taasisi za umma huko nyuma. Sikumbuki namna yoyote ambayo inawezekana benki kumlipa mtu binafsi interest (riba) ya fedha zilizowekezwa na sekta ya umma. Nasema sikumbuki, sijawahi kuona na sikuwahi kufanya hivyo,” alisema Mafuru.

  “Lakini kama kuna practice (vitendo), watu wana-develop (wanaanzisha) uhalifu, kama imetokea itagundulika. Kwa taarifa yenu tu, kutokana na hili jambo, tulianza mwezi uliopita tukiwa Dodoma kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali na uamuzi tuliouchukua ni kufanya ukaguzi maalumu. Kwa hiyo CAG anapewa jukumu la kukagua.”

  Alisema uchunguzi huo umeanzia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ili kujiridhisha kwa sababu hizo ni tuhuma tu.

  “Kwa hiyo kama hizo tuhuma ambazo mheshimiwa Rais amezisema kwamba kuna ma-Chief Executive Officers (maofisa weatendaji wakuu) wamekuwa wakichukua, ukaguzi umeanza. Muda si mrefu tutajua mbivu na mbichi,” alisema Mafuru.

  Huku akitoa mfano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo pia Rais Magufuli aliitaja kuwa na fedha kwenye akaunti maalumu, Mafuru alisema akaunti yake ya mwisho inaiva mwezi huu (Novemba) na hawakuona sababu ya kuifunga kwa sababu wangepoteza faida.

  “Lakini nyingi ziko benki nyingine zitakuwa zinaiva. Kwa sababu zipo zenye mitaji ya mabilioni ya shilingi. Sasa uamuzi wa busara ni upi? Kuivunja na kupoteza ulichopata au kuiacha ikomae?” alihoji.

  “Maelekezo ya Rais ni kututaka sisi na mashirika haya kuhakikisha kuwa utaratibu huu uliojengeka, unabadilika. Ilikuwa hivyo huko nyuma, haikuwa dhambi lakini sasa utaratibu umebadilika.”

  Alisema uamuzi wa kuhamishia fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulianzia mwaka huu na mpaka Septemba walikuwa wamerudisha Sh515 bilioni kwa mashirika 218.

  “Kwa jinsi ambavyo mashirika ya umma ambayo yamekuwa yakiendeshwa huko nyuma, haikuwa rahisi kwa Serikali kupata jumla ya fedha zinazokusanywa. Kwa hiyo sababu ya kwanza iliyoisukuma Serikali ni kwamba mapato ya Serikali yajumlishwe mahali pamoja,” alisema.

  “Tungekuwa tunapiga simu kila shirika na kuuliza, Tanapa mna shilingi ngapi benki fulani, isingekuwa rahisi. Tukasema, kwa maana ya mapato, tutakusanya sehemu moja yaani Benki Kuu, kwa utaratibu huu mimi nikitaka kujua mashirika ya umma yamekusanya kiasi gani, nitasema bila shaka.”

  Alisema malalamiko kwamba Serikali imeondoa fedha kutoka benki za biashara na kuzipeleka BoT hayana msingi, kwa sababu ni sehemu ya mfumo wa benki.

  “Kuna watu wanasema Serikali imezichukua fedha hizo imezipeleka kwenye mfuko mkuu. Hilo jambo haliwezekani na ni kinyume cha sheria. Tanesco wakitaka fedha wanaiandikia benki wanasema ziende CRDB, ziende NBC ziende benki Z kwa ajili ya kufanya matumizi yao,” alisema.

  “Kwamba fedha zimechukuliwa, kumekuwa na ukata, hilo jambo haliwezekani. Kwa taarifa yenu, hata Benki Kuu ikiona kuna uhitaji wa fedha kwenye soko wanafanya hivyo kwa kutoa mikopo kwa benki. Benki kwa benki zenyewe zinakopeshana,” alisema.

  Alitaja sababu ya pili kuwa ni Serikali kukataa kukopa fedha zake yenyewe.

  “Maana yake ni kwamba, ile gharama ya kukopa ni matumizi ya Serikali. Sasa sisi tumejiuliza kwa nini tukope fedha zetu wenyewe? Kwa hiyo ili kupunguza matumizi haya ya kukopa, tumesema zihame zije huku. Tunaamini tunaweza kuzikopa Benki Kuu kwa bei nafuu,” alisema.

  Sababu ya tatu ni kwa taasisi za Serikali zinazotegemea ruzuku kwa asilimia 100 kuficha fedha hizo kwenye akaunti za muda maalumu.

  “Sasa ugomvi wa Rais Magufuli unakuja hapa. Wewe umekuja ukasema una mahitaji ya msingi, unataka kuyatekeleza, ukapewa pesa, kabla ilikuwa tupeleke pesa Muhimbili, ilikuwa tupeleke Wizara ya Elimu. Tukasema tukupe wewe, kumbe hujamaliza mchakato wako wa manunuzi. Sasa kama una miezi sita bado, kwa nini unataka sasa hivi?” alihoji Mafuru.

  “Kwa hiyo Rais anapata taarifa kwamba tulimnyima Msajili wa Hazina, lakini, tumempa labda TRA Sh120 milioni, tulidhani anakwenda kuitumia labda matumizi yake ya miezi miwili mitatu. Kumbe ameziweka kwenye akaunti ya muda maalumu. Unajua kuweka kwenye akaunti hiyo ni kuonyesha kuwa una ziada.”

  “Tunapotosha na kusema ‘fixed deposit account’ ni tatizo, hoja ni ile tabia ya kuweka fedha ambazo zingeweza kutumika kwenye miradi mbalimbali, lakini ni bidhaa halali kabisa kwa benki kwa ajili ya kuwawezesha wale wenye fedha za ziada wazihifadhi,” alisema.

  Fedha katika mzunguko

  Kuhusu malalamiko ya ukosefu wa fedha katika mzunguko, Mafuru alisema ni kutokana na fedha kwa nyingi kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

  “Kupanga ni kuchagua, sisi kama nchi tumechagua kwamba, badala ya kupeleka fedha kwenye matumizi ya kawaida ambayo ingeshuka chini kwenye mzunguko, tumetumia kwenye miradi ya maendeleo ambayo matokeo yake hayaonekani sasa hivi,” alisema.

  Alisema sababu ya kudorora kwa baadhi ya benki nchini ni kutokana na mikopo kuharibika. Alisema mpaka sasa benki zimekopesha zaidi ya Sh16 trilioni na Sh1.43 trilioni ni mikopo isiyolipika na ndiyo sababu ya kuyumba.

  “Tatizo wenye benki hawasemi ukweli, hivi Sh515 bilioni zilizohamishwa na Sh1.43 trilioni walizokopa, zipi nyingi?” alihoji.

  Maoni ya wasomi

  Wakizungumzia suala hilo baadhi ya wasomi wameonyesha wasiwasi wa hatua za Rais Magufuli kuhusu akaunti ya muda maalumu kwa watendaji wa Serikali.

  Profesa wa Uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema akaunti hiyo si tatizo na haiwezekani watendaji kuitumia kuiba fedha za umma.

  “Hata mimi nashindwa kuelewa ni kwa namna gani watendaji wa Serikali wanaweza kuziiba, kwa sababu Sheria ya Fedha imeelekeza, kuna wakaguzi wa ndani na nje na hata CAG. Sioni kwa vipi watu watazitoa,” alisema Profesa Ngowi.

  Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema hatua alizochukua Rais Magufuli zinawezekana kuwa ni hisia za rushwa.

  “Anakuwa na hisia kwamba akaunti hizo ndizo zinatumiwa kuchota fedha au kutumika kwa rushwa,” alisema.


  No comments:

  Post a Comment

  Siasa

  Michezo

  Udaku